Ukame unavyotishia njaa, magonjwa kwa wananchi

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Misimingori wakiwa kwenye foleni kupata mgawo wa maji wa ndoo mbili kila kaya kupunguza makali ya uhaba wa maji wanayokabiliana nayo iliyosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi. Picha na Bertha Ismail

Muktasari:

  • Ni mateso!.. ndivyo unavyoweza kusema unaposhuhudia wananchi wa Monduli wanavyosota usiku na mchana kusaka maji kwenye mabwawa machache yaliyobakia baada vyanzo vingi tegemezi kukauka kutokana na hali ya ukame, iliyoikumba wilaya hiyo iliyoko mkoani Arusha.

Monduli. Ni mateso!.. ndivyo unavyoweza kusema unaposhuhudia wananchi wa Monduli wanavyosota usiku na mchana kusaka maji kwenye mabwawa machache yaliyobakia baada vyanzo vingi tegemezi kukauka kutokana na hali ya ukame, iliyoikumba wilaya hiyo iliyoko mkoani Arusha.

Monduli yenye vyanzo vya maji zaidi ya 90 ikiwemo chemchem, mito, visima na mabwawa, vingi vimekauka kutokana na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha mateso kwa wananchi likiwamo kubwa la ukosefu wa maji, chakula na malisho.

Adha hiyo inawapata zaidi wanawake na watoto wanaokwenda kutafuta maji mwendo wa zaidi ya kilomita 15 hadi 20 huku wakikabiliana na hatari mbalimbali ikiwemo wanyama wakali kama tembo, fisi, simba na wanaume wenye tabia ya kufanya vitendo vya ubakaji na ulawiti.

Mwenyekiti wa Kijiji Cha Nanja, Yamati Lemomo alisema, “Ukame umekuwa tishio kubwa kwetu, hatujapata mvua za kutosha miaka ya hivi karibuni, mbaya zaidi mwaka jana hatujapata kabisa, kwani mvua iliyopaswa kunyesha Novemba hadi Januari, kabla ya kukatika na kuendelea tena Machi hadi Juni hazijanyesha zaidi ya kupata manyunyu kidogo Machi” alisema Lemomo.

Alisema ndiyo sababu vyanzo vingi vya maji vimekauka.“Maji yanayopatikana mbali pia ni machafu hayafai kwa matumizi ya binadamu, lakini hakuna namna wananchi wanalazimika kuyatumia.

Naye Naserian Mebukori mmoja wananchi wa eneo hilo, alisema kuwa wanatumia muda mwingi kusaka huduma maji badala ya shughuli za kimaendeleo, ikiwamo wanafunzi kukosa masomo kwa kupeana zamu ya kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

“Tunapitia mateso makubwa kutokana na mabwawa yetu tunayotegemea hapa kama Kilotorok na Lesimingori kukauka, hivyo tunalazimika kufuata maji zaidi ya kilomita 15 katika bwawa pekee lililobakia la Nanja. “Hata hivyo maji yanayopatikana ni machafu tunalazimika kuchanganya na unga wa ugali au majivu kisha tunayaacha yatulie ili tope lijichuje kwenda chini ndio yafae kwa matumizi, lakini hakuna chaguo tunayatumia hivyo hivyo.

Moja ya mabwawa yaliyokauka Monduli 'Sogea' kutokana na ukame. Picha na Bertha Ismail

Alisema hukusanya wanawake wenye uhitaji wa maji siku hiyo pamoja na watoto kwa ajili ya kuamshana saa tisa usiku kuyafuata katika bwawa la Nanja na kurudi asubuhi saa tatu au nne, lengo ni kukabiliana na hatari za njiani ikiwemo wanyama wakali lakini pia matukio ya ubakaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Lepurko, Lendo Melembuki alisema kuwa kijiji hapo kuna zaidi ya wananchi 1,138 wanategemea maji kutoka bwawa la Losikito ambalo limekauka tangu Julai kutokana na mmomonyoko wa udongo uliosababishwa na ukame, hali inayowaweka wanachi wake kwenye taabu ya kusaka maji ambayo pia siyo salama.

Akilizungumzia hilo, Isaka Mollel alisema kuwa tatizo la ukame limekuwa kubwa kwa wananchi wa Kata ya Sepeko na Lepurko kwani hata wanyama wakali wanatoka mafichoni na kuja kwenye makazi ya watu kusaka maji hali inayowaweka kwenye hatari kubwaya kushambuliwa.

“Tunaomba Serikali na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) lituokoe kwenye hili, kwani wamekuwa wakidhuri watu na zaidi fisi wanakula mifugo yetu,”alisema.

Alisema, “N’gombe wengi wamekufa, achilia mbali mbuzi na kondoo kwa sababu ya kukosa malisho. “Tumehamisha mifugo na kubakisha mbuzi ambao wamekonda sana na tunabadilidilishana na madebe mawili ya mahindi kwa wafanyabiashara wanaotoka mikoani kuja mnada wa Mto wa Mbu hii ni kusaidia watoto wetu wapate angalau mlo mmoja” alisema.

Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Lepurko wakisaidiana na mafundi wa RUWASA kuunganisha maji kutoka kwenye gari kwenda kwenye matenki kwa ajili ya kuwagawia wananchi wa Kijiji hicho Kila kaya ndoo 2, kwa matumizi ya kunywa Ili kukabiliana na hali ya ukame iliyoikumba. Picha na Bertha Ismail.

Naye Mzee Isack Kismo alisema hofu waliyonayo kwa sasa ni magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuhara, kuumwa matumbo, na magonjwa ya ngozi kutokana kutumia maji machafu.

“Kuoga!!!.. Ndugu mwandishi unaongelea kuoga? Kwetu hiyo ni anasa kama zingine, sisi wanaume hatujui mara ya mwisho tumeoga lini zaidi ya wanawake ndio tunaona wanaoga angalau kila wiki mara moja,” alisema Kismo.

Alisema ukame huo umetengeneza fursa kwa watu wenye uwezo kifedha, wamenunua matenki na kukodisha magari ya boza na kwenda kusomba maji masafi jijini Arusha na kwenda kuwauzia Sh1,000 kwa ndoo ya lita 20.

Akizungumzia hali hiyo, Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini ‘Ruwasa’, Neville Msaki alisema wameiona hali hiyo na wameanza kusambaza maji kwa kutumia magari (maboza) kwa ajili ya kuwapa afueni wananchi. “Tulifanya tathmini na kugundua vijiji vinane kati ya 62 vya wilaya nzima ndio waathirika wakubwa wa vyanzo vyao vyote vya karibu vya maji kukauka, tuliomba fedha Serikali kuu kupitia waziri wa maji na tukapewa Sh100 milioni kwa ajili ya kutekeleza mpango huo wa dharura”alisema Msaki.

Alitaja vijiji vilivyoathirika zaidi na vilivyoanza kupatiwa maji ya dharura kuwa ni Arkatan, Arkaria, Mti mmoja, Nanja, Lepurko, Losimingori, Engaroji, na M’buyuni. “Tumeomba maji mamlaka ya Maji safi Arusha (AUWSA) na kusambaza katika matanki 20 ya lita 5,000 kila moja tuliyoyasambaza katika vijiji hivyo, ambapo kila siku lita 60,000 hupelekwa kwa magari na ni utaratibu utakaodumu kwa mwezi mmoja tunatarajia baada ya kipindi hicho mvua zitakuwa zimeshaanza,”alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe alisema wametambua changamoto za wananchi wake wanayopitia ikiwemo uhaba wa maji, chakula na malisho ambapo wameanza kuchukua hatua za haraka za kuwasaidia, ikiwamo kuwasambazia maji.