Wanyamapori waanza kufa Burunge kwa kukosa maji

Askari wa Burunge WMA wakiokoa mnyama ambaye amezama kwenye tupe baada ya kukosa maji. Picha Mussa Juma

Muktasari:

Mabadiliko ya tabia nchi yameanza kusababisha kukauka kwa mito na vyanzo vya maji maeneo kadhaa nchini.

Babati. Idadi ya Wanyamapori imeanza kutaabika na baadhi kufa kwa kukosa maji katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (WMA), Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara

 Burunge WMA ipo kati ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Manyara na inaundwa na vijiji 10 ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 24,319.

Licha ya wanyamapori kuanza kufa pia kumeongezeka matukio ya ujangili na migogoro baina ya wananchi na wanyamapori kutokana na wanyamapori hao kuanza kuingia maeneo ya vijiji kusaka maji na malisho.

Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaisej akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Oktoba 25, 2022 amesema wanyamapori wameanza kufa kutokana na kukosa maji na kuzama kwenye tope kutokana na ukame.

"Hali ni mbaya sana ya ukame kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, tumeanza kupata kesi za wanyama kufa, wengine kuzama kwenye tope wakitafuta maji na wengine kuingia vijijini," amesema

Hata hivyo, ili kukabiliana na hali hiyo katika eneo la Kitalu cha uwindaji kinachomilikiwa  na Taasisi ya EBN kilichopo ndani ya Burunge WMA wamechimba mabwawa kusaidia maji kwa mifugo.

Meneja Uhusiano wa EBN, Charles Sylvester amesema wameamua kuchimba mabwawa na kutoa maji kwa Wanyamapori ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani maji yamepungua.

"Hivi Sasa eneo letu kuna idadi kubwa ya Wanyamapori tofauti na miaka ya nyuma kabla ya kupewa kitalu hiki ambapo pia sasa wanyamapori wamekuwa rafiki na watu na kuwezesha utalii wa picha," amesema

Mwenyekiti mstaafu wa serikali ya kijiji cha vilima vitatu, Erasto Belela amesema athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kubwa lakini mahusiano mazuri baina ya vijiji na mwekezaji EBN imesaidia kupunguza athari.