Ukatili unavyochangia magonjwa afya ya akili

Muktasari:
- Wakati matukio ya ukatili dhidi ya watoto na mauaji ya wenza yakiendelea kushika kasi nchini, watafiti kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) wamethibitisha kuwepo uhusiano wa kisayansi wa matatizo ya afya ya akili na vitendo vya ukatili.
Dar es Salaam. Wakati matukio ya ukatili dhidi ya watoto na mauaji ya wenza yakiendelea kushika kasi nchini, watafiti kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) wamethibitisha kuwepo uhusiano wa kisayansi wa matatizo ya afya ya akili na vitendo vya ukatili.
Mfululizo wa tafiti zilizofanywa na idara ya magonjwa ya akili umethibitisha hilo, huku kukiwa na wasiwasi kuwa hatua zisipochukuliwa hali itakuwa mbaya zaidi, kutokana na kuwepo watu wengi wenye matatizo hayo bila kujitambua.
Hadi sasa inaonekana ni asilimia 20 pekee ya wenye matatizo ya afya ya akili ndio wanatafuta matibabu, huku asilimia 80 iliyobaki wakiwa hawajitambui.
Tafiti zinaeleza kuwa miongoni mwa wanaojitambua wanatafuta tiba mbadala, ikiwemo dawa za kienyeji na maombi kwenye nyumba za ibada.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Mkuu wa idara ya afya na magonjwa ya akili Muhas, Dk Ester Mzilangwe anasema ukatili unaosababishwa na afya ya akili unazidi kuongezeka kutokana na watu wengi wenye matatizo hayo kutoelewa hali zao.
Anasema wengi wanaofanya vitendo vya ukatili kwa kuwashambulia, kuwadhuru wengine au hata kujidhuru wenyewe ni matokeo ya kukosa utatuzi au ufumbuzi wa changamato zinazowakabili.
Akieleza matatizo hayo namna wengi wanavyoyapata anasema ni kutokana na mazingira wanayokulia, changamoto wanazopitia na namna wanavyokabiliana nazo.
“Kuna mambo mengi yanayomfanya mtu kufanya ukatili, ila hakuna mtu anazaliwa mkatili, watu hujifunza kutatua matatizo yao kwa kufanya ukatili. Tafiti zinaonyesha kuwa wengi waliofanya ukatili wameshuhudia vitendo vya ukatili vikifanywa mbele yao wakiwa watoto.
“Hapa tunamzungumzia yule mtoto ambaye anaona baba akimpiga mama pale kunapokuwa hakuna maelewano, au mama akimtolea maneno machafu baba na mambo kama hayo, hii inamfanya mtoto aone kwamba tatizo lililo mbele yake linaweza kutatuliwa kwa kufanya ukatili au kumuumiza mwingine,” anasema.
Anasema Chanzo kingine cha hali hiyo ni tamaduni ambapo katika jamii nyingi hasa za Kiafrika mwanamume anajengewa mawazo kuwa yeye ni kichwa cha familia, pale inapotokea mambo kuwa kinyume na imani hiyo nguvu na mabavu yanaweza kutumika kulazimisha.
“Jamii inamlea mwanamume kuwa mfanya maamuzi, mtoa amri yaani yeye ndio kila kitu kwenye familia, asipokuwa hivyo anaangaliwa kwa jicho tofauti na ndipo shinikizo linapoanzia. Sasa wakati mwingine anaweza kutumia ukatili ili kuonyesha uanaume wake.
“Tatizo lingine ni wanawake kukubali vitendo vya ukatili, wenyewe wanaona ni kawaida kumbe hata hilo ni tatizo la afya ya akili. Mara nyingi huwa tunakutana na wagonjwa wa aina hii, yaani anaishi kwenye ukatili lakini yeye anaona ni kawaida au ndio upendo, ila ukweli ni kwamba hili ni tatizo la afya ya akili na anayefanya ukatili naye ana tatizo, kwa hiyo hapo ni bomu linalotengenezwa na kulipuka kwake ndio matukio kama haya tunayasikia,” anasema Dk Ester Mzilangwe.
Nini kinaendelea kwenye ubongo wa mtu anayefikia kumuua mwenza?
Dk anafafanua kuwa wapo ambao tayari wana ugonjwa wa akili ambao unamsukuma kumdhuru mwingine kwa lengo la kujihami pale anapohisi anataka kufanyiwa kitu kibaya, na hii hutokea mara chache.
Anabainisha kuwa hali hii inatokana na kutokuwepo mawasiliano ambayo yanatengenezwa kupitia mazungumzo na makubaliano ya wenza wenyewe.
“Kitu kikubwa kwenye uhusiano ni mawasiliano, lakini unakuta wengine hawana namna nzuri ya kuwaelewesha wenza wao, hapa sasa ndio kila mmoja atashika njia yake na kufanya kila anachoona ni sawa kwake.
“Tabia inaanza kidogo kidogo, ukifuatilia yalipotokea matukio ya ukatili kwa wenza utagundua haikuanzia siku hiyo, yanaanza taratibu na hatua zisipochukuliwa itaonekana kawaida na anayefanya hivyo ataongeza kile anachofanya,” anasema.
Hali ikoje kwa sasa
Dk Ester alisema matukio ya vitendo vya ukatili yanayotokana na afya ya akili yamekuwa yakiongezeka na hii ni kutokana na watu kuanza kuwa na uelewa wa kina na kutoa taarifa pale yanapotokea.
“Bado hatujafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzuia, ila jamii imeanza kuelewa kuhusu vitendo hivi na vinapotokea taarifa zinatolewa, vyombo vya habari vinafanya kazi kubwa, tunaona polisi nako kuna dawati la kijinsia watu wanakimbilia huko kutoa taarifa, naweza kusema ni hatua kubwa ingawa bado tunatakiwa kuongeza nguvu ili kuzuia.
“Kingine napata faraja kubwa kuona baadhi ya watu wanatafuta msaada wa kimatibabu, unaweza kuwa hospitali ukaletewa watoto uzungumze nao ili kuona kama amefanyiwa ukatili au la baada ya mzazi au mlezi wake kuwa na wasiwasi,” alisema.
Pamoja na hatua hizo, unyanyapaa inabaki kuwa changamoto kubwa na kikwazo kinachowafanya watu wengi wenye matatizo ya afya ya akili washindwe kutafuta matibabu sahihi kwa kuhofia jamii itawatazama vibaya.
Akizungumzia hilo, Dk Ester alisema: “Unyanyapaa ni changamoto kubwa ambayo ipo kwenye jamii na inasababisha watu washindwe kutafuta matibabu sahihi, matokeo yake wanaishia kwenye maombi, mtu anaona akienda hospitali kitengo cha magonjwa ya akili ataonekanaje. Wapo pia ambao wanawatolea maneno ya dharau watu wanaojaribu kutafuta matibabu na kusababisha wakate tamaa au kuacha kutibiwa,” anafafanua Dk Ester.
Muhas yajitosa kulishughulikia suala hili kisayansi
Akizungumzia walivyojipanga kukabiliana na tatizo la afya ya akili, Mkurugenzi wa tafiti na machapisho wa Muhas, Profesa Bruno Sunguya anasema suala hilo limeingia kwenye vipaumbele vya Muhas na ndiyo sababu limekuwa mada kuu kwenye kongamano la kisayansi linalofanyika Julai 14 na 15 mwaka huu.
Profesa Sunguya anasema kwa kawaida mada kuu katika kongamano hilo ambalo linafanyika kwa mara ya 10 sasa, hubebwa na tatizo ambalo limetikisa jamii, kwa mwaka huu suala la ukatili hasa kwa wenza na watoto ndilo limechukua nafasi kubwa.
“Suala la ukatili limekuwa kubwa na ndiyo maana tumeona hebu wanasayansi tufanye kazi yetu tunaweza kusaidia kwa kiasi fulani, na tumeona kuna uhusiano mkubwa wa ukatili na afya ya akili, hivyo kupitia kongamano hili la tafiti mbalimbali zitawasilishwa katika eneo hilo na tutatoka pale na mtazamo wa kisayansi.
“Baada ya hapo tutaandaa kongamano lingine litakalohusisha wadau mbalimbali katika jamii, tuwaeleze kilichopo na kwa pamoja tutajadiliana tunakwendaje kulinusuru Taifa dhidi ya janga hili.
“Kisha kutakuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu afya ya akili ambao tutashirikiana na wizara ya afya kuuandaa na hapo ndipo utazinduliwa mkakati wa kitaifa wa afya ya akili. Hii ina maana kongamano la kisayansi ni hatua ya kwanza katika safari ndefu ambayo tumeianza kukabiliana na changamoto hii,” anasema Profesa Sunguya.