Ukiukwaji wa haki za binadamu wakanushwa

Islamabad. Imeelezwa kuwa jimbo la Balochistan nchini Pakistan inafanyika operesheni kubwa ya kijeshi ambayo pamoja na mambo mengine, yameripotiwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Kwa mujibu wa mtandao wa Dawn, Bunge la Balochistan lilipitisha sheria ya kupambana na ugaidi inayotajwa kuzua wasiwasi mkubwa wa utekelezaji wa haki za binadamu huku ikitoa mamlaka ya vyombo vya kutekeleza sheria kuwaweka watu kizuizini kwa kipindi cha miezi mitatu bila kufunguliwa mashtaka.
Mtandao huo unaeleza kuwa kiongozi wa Tume ya Baloch Yakjehti (BYC), Dk Mahrang Baloch pamoja na wanaharakati wengine wanasota gerezani na kumekuwa na ripoti kwamba huenda wakakumbana na kifungo.
Makundi kadhaa ya haki za binadamu na wanasiasa wa nchini Pakistani wameibua wasiwasi kuhusu sera mpya za Balochistan kwamba ni mwiba kwa wananchi.
‘’Matukio ya kutoweka kwa watu, mauaji ya waandishi wa habari, wanaharakati na watu mbalimbali yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika miezi ya hivi karibuni,’’ alisema Dk Baloch
Akielezea wasiwasi wake juu ya matukio ya hivi majuzi huko Balochistan, seneta wa zamani na kiongozi wa kitaifa wa Pashtun, Afrasiab Khattak alisema kuna umuhimu wa kuzibiti vikundi tishio kwa ugaidi.
‘’ Ni ishara tosha kwamba jeshi la Pakistan linacheza mchezo hatari dhidi ya makundi ya waasi wa eneo la Baloch ili kuyumbisha jimbo hilo lenye utajiri wa madini,’’alisema Khattak.
Aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Afghanistan, Zalmay Khalilzad alidai vikosi vya usalama vya Pakistan ni kama vinaungana na vikundi vya Baloch jambo alilodai kuwa ni hatari zaidi.
Hata hivyo, mamlaka nchini Pakistan zimekuwa zikisisitiza kuwa mambo hasi dhidi ya Taifa hilo yanachochewa na waasi.