Prime
Ulemavu wa ajabu unaoitesa famili hii
Muktasari:
- Si adhabu bali ni majaliwa yake Mola.Ndivyo unavyoweza kusema kwa yaliyomkuta Nighenjijwe Joseph Mgonja (67) mkazi wa kijiji cha Gwang'a, kata ya Chome wilayani Same, baada ya kuzaa watoto watano wenye ulemavu wa viungo unaofanana.
Same. Si adhabu bali ni majaliwa yake Mola.Ndivyo unavyoweza kusema kwa yaliyomkuta Nighenjijwe Joseph Mgonja (67) mkazi wa kijiji cha Gwang'a, kata ya Chome wilayani Same, baada ya kuzaa watoto watano wenye ulemavu wa viungo unaofanana.
Watoto hao ambao hawajiwezi kwa lololote walizaliwa na ulemavu wa viungo na tangu wazaliwe, hawajawahi kuongea wala kutembea kutokana na ulemavu walionao.
Zaidi, wanatambaa kwa mikono, huku wakiburuza miguu, huku wakishindwa kujua lugha yoyote licha ya wao wenyewe kuelewana kwa lugha ambayo mtu baki hawezi kuijua.
Mama huyo mjane, alibahatika kupata watoto wanane, wakiwemo hao watano.
Anasema kila alipojaribu kubeba ujauzito alikuwa akizaa mtoto mwenye ulemavu na mpaka alipofikisha watoto watano na bado hakukata tamaa mpaka hapo alipobarikiwa watoto watatu ambao sio walemavu.
Anasema licha ya changamoto alizopitia hakuwahi kukata tamaa na jamii haikumnyanyapaa zaidi ilimtia moyo na kumuonea huruma.
Anasema kila alipojifungua mtoto mwenye ulemavu alizunguka hospitali zote za Wilaya na Mkoa na kwamba wataalam wa afya waliwafanyia watoto wake vipimo na hawakubaini aina yoyote ya ugonjwa.
"Nilizunguka nao hospitali zote wakanambia hawana ugonjwa wowote,’’ anasema.
Anaongeza: "Ni ngumu kulea watoto wote hawa wakiwa na matatizo haya lakini jamii haikuniacha, wananipa msaada... ‘‘
Jirani yake, Nasembamakaa Mgonja anasema mama huyo anawalea wanawe kwa tabu kutokana na changamoto waliyonayo.
"Wakati mwingine unaweza kuwakuta wanalia tu kutwa nzima, wanahitaji msaada wa kila namna kwa kweli,’’ anasema.
Mtendaji wa Kijiji.
Niwael Mgonja anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, wanashirikiana na familia hiyo kuhakikisha wanakuwa katika mazingira rafiki na kupunguza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
‘‘Tayari Serikali imewakatia bima ya afya ili pale wanapougua waweze kupata huduma za haraka na zisizo na usumbufu za afya,” alisema.