Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Ulemavu unavyoitesa familia ya Mallya

EXCLUSIVE: Ulemavu unavyoitesa familia ya Mallya, waomba msaada

Muktasari:

  • Hujafa hujaumbika, usemi huu unaweza kuutumia kuelezea milima na mabonde anayopitia Edmund Mallya, ambaye katika umri wake wa miaka 68 hakufikiria siku moja angepata ulemavu na kuwa tegemezi.


Dar es Salaam. Hujafa hujaumbika, usemi huu unaweza kuutumia kuelezea milima na mabonde anayopitia Edmund Mallya, ambaye katika umri wake wa miaka 68 hakufikiria siku moja angepata ulemavu na kuwa tegemezi.

Edmund ni baba wa watoto watatu, alipatwa na ulemavu Oktoba mwaka 2021 baada ya mguu wake wa kushoto kukatwa kutokana na kushambuliwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa kisukari.

Kabla ya hapo Mallya alikuwa ndiyo tegemeo kwa familia yake, mkewe na mtoto wake wa mwisho pia ni walemavu.

Kupitia kazi ya udereva aliweza kupata kipato kuhakikisha familia yake inapata mahitaji yote ya muhimu wakiishi kwenye nyumba ya kupanga jijini Dar es Salaam.

Mwananchi ilifika katika nyumba wanayoishi wanafamilia hawa ambapo Mallya anasema licha ya umaskini alionao, alijimudu kuihudumia familia yake tofauti na hivi sasa anajiona ni mzigo.

“Mke wangu ni mlemavu, mwanangu wa mwisho pia ni mlemavu, hata hivyo hali zao hazikuwahi kuwa shida kwangu, niliishi nao kwa upendo mkubwa, watoto wangu wawili ni wazima lakini hawana kazi hivyo tunaishi kwa kutegemea kudra za Mungu,” alisema.

Mallya anaeleza kuwa ulemavu aliopata uzeeni unamfanya apoteze dira ya maisha na matumaini ya kuishi kutokana na ugumu wa maisha akikabiliwa na changamoto lukuki zinazomfanya akate tamaa ya kuishi.

Anasema ugonjwa wa kisukari haujaishia katika mwili wake, licha ya kuchukua mguu wake mmoja lakini hivi sasa unatishia kuondoa na wa pili iwapo atashindwa kutumia dawa alizoandikiwa.

Huku akilengwa na machozi, Mallya anasema daktari amemueleza apate dawa ili kunusuru mguu wake mwingine usikatwekwa sababu ugonjwa tayari umeshaingia mwilini.

“Kuna dawa ambazo daktari aliniandikia nitumie, dawa hizo zinauzwa Sh253,000, sina uwezo wa kumudu hizo gharama hivyo nimekaa nikisubiri kuona mguu wangu mwingine nao ukiondoka,” anasema.

Sanjari na hilo, kichwa chake kinawaka moto ni wapi hasa atapata kodi kwa ajili ya nyumba anayoishi na familia yake, maana tangu akatwe mguu hadi sasa anadaiwa kodi ya miezi sita.

“Mwenye nyumba ni mvumilivu, ametuvumilia katika kipindi chote cha miezi sita maana kodi yangu iliishia Desemba mwaka jana, lakini najiuliza atavumilia hadi lini na yeye ni binadamu itafika wakati atachoka, je, hilo likifika nitafanya nini,” anasema Mallya huku akizuia machozi kudondoka.

Anaomba bajaji

Mallya anaamini kuwa bado ana uwezo wa kuendelea kuwepo barabarani hivyo ombi lake ni kusaidiwa aweze kupata bajaji ili afanye biashara kuepukana na adha ya kuwa ombaomba.

Mkewe, Amina Hassan kiliochake mustakabali wa maisha ya mtoto wao Joachim ambaye amezaliwa na matatizo tangu mdogo, lakini hali ya ulemavu ya mama yake na uwezo duni wa familia vilichangia ulemavu wake.

Amina ambaye pia ni mlemavu anasema anaumia kuona mtoto wake naye maisha yake yatakuwa kwenye umaskini wa kutupwa kutokana na hali aliyonayo.

Historia ya ulemavu wa mama huyu ilianza akiwa mtoto mdogo baada ya kuugua ugonjwa wa polio uliomfanya kupooza upande mmoja.

Pamoja na hali hiyo, Amina anasema mama yake alipambana kuhakikisha anapona lakini hata hivyo tayari changamoto ilishaingia kwenye mwili wake na hatimaye akakubaliana na hali.

“Kwa kuwa mama yangu alikuwa mzima alipambana kwa kila hali kuhakikisha nakuwa sawa ila ikaonekana kimatibabu imeshindikana tayari nilishapata ulemavu, ikabidi aishi na mimi kulingana na hali yangu.

“Pamoja na hali hiyo nilipata haki zote za msingi ikiwemo kupata elimu, nilisoma shule ya msingi na hatimaye nikaenda sekondari ya ufundi ambako nilimaliza kidato cha nne nikiwa na taaluma ya ufundi bomba.”

Kama ilivyo kwa mabinti wengine alipomaliza masomo yake alibahatika kupata kazi na hatimaye Mallya akamposa na kuanzisha naye familia ambayo hadi sasa ina watoto watatu.

Maisha yalikuwa ya kawaida tu nafanya shughuli zangu pamoja na hali niliyokuwa nayo, nikazaa watoto wawili wazima kabisa, tabu ilianza alipozaliwa Joachim.”

Mtoto huyu alizaliwa miaka 16 iliyopita, nilimzaa akiwa njiti na hadi narudi naye nyumbani sikujua kama ana tatizo kubwa zaidi ya kuzaliwa kabla ya muda.

Nilikuja kugundua ana mtindio wa ubongo baada ya kutoelewa makuzi yake, nilipomrudisha hospitali ndiyo nikaambiwa hivyo, kana kwamba hiyo haitoshi nikagundua hata miguu yake ni mizito.”

Baada ya kumpeleka hospitali akaelekezwa sehemu kwa ajili ya kumpeleka mtoto wake kufanya mazoezi ambayo yangemsaidia kutambaa na hatimaye kutembea.Hakujali hali aliyokuwa nayo Amina alisimama kwenye jukumu lake la umama na kumbeba mwanae kumpeleka kwenye kituo hicho cha mazoezi yake hadi alipoanza kutambaa.

Kinachoumiza kichwa chake ni mtoto huyo kukosa haki ya kusoma kwa kuwa alijaribu kumpeleka katika shule kadhaa za jirani wakamwambia hawawezi kumchukua kutokana na hali aliyonayo, hakuna miundombinu inayoweza kumfanya awe vizuri.

Kauli ya daktari

Kulingana na Dk Isack Maro ugonjwa wa polio au kwa kitaalamu Poliomyelitis ni wa kihistoria uliofahamika sana miaka ya zamani kutokana na athari zake mbaya.
Miaka ya hivi karibuni umekuwa hausikiki sana kutokana na uwepo wa chanjo dhidi yake, ambayo imefanya kazi kubwa ya kuutokomezea. Kutokana na ugunduzi na utoaji wa chanjo ya polio mwaka 1979 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa ugonjwa huo umeondoka kabisa duniani.
“Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosambaa kwa kasi. Unasababishwa na viini vya maradhi aina ya virusi vinavyoitwa virusi vya polio. Ugonjwa huu husababisha madhara makubwa kwenye mwili wa mwanadamu yakiwamo madhara kwenye mishipa ya fahamu yanayosababisha mgonjwa kupooza yaani paralysis.


“Pia huambukizwa kwa kugusana na mtu mwenye ugonjwa huu, kula au kunywa kinywaji chenye virusi vya polio. Kwa kupitia kinyesi” anasema

Kwa watakaguswa kumsaidia Mallya na familia yake mawasiliano ya mkewe ni 0682374977