Ulevi wakithiri Moshi, vijana wadaiwa kushindwa kuoa

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Moshi anakusudia kutangaza operesheni ya siku 21  kupamana na wauzaji na wanywaji wa pombe muda wa kazi.

Moshi. Ukistaajabu ya musa utaona ya firauni. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema, baada ya baadhi ya wanaume waliofikia umri wa kuoa Kijiji cha Singa, Kata ya Kibosho Mashariki, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kutooa  kutokana na kuathiriwa na ulevi.

Mbali na kuoa, hata wale wenye wake wanadaiwa kushindwa kuhudumia ndoa zao na kupata watoto hali ambayo imechangia ongezeko la migogoro ya ndoa na nyingine kuvunjika. 
Hali hiyo imesababisha kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa na kufanya baadhi ya makanisa kukosa watoto wa kubatiza, hali inayosababisha idadi ya watoto wanaobatizwa kushuka kutoka watoto 100 hadi kufikia wanane.

 Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Machi 25, 2024 na Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kibosho, Padri Beatus Vumilia wakati wa ufunguzi wa zahanati mpya ya Matela iliyopo katika kijiji hicho.

Amesema imefika mahali jamii imeshindwa kujitawala na kutawaliwa na pombe na kushindwa kutimiza wajibu wa kijamii na kwamba imefikia mahali kanisa linakosa watoto wa kubatiza.
"Kumekuwepo na changamoto baada ya jamii kuporomoka katika malezi na maadili hata katika suala la uzao nalo limepungua sana, limeathiri sana hata katika wale watoto wanaoingia katika malezi ngazi za mafundisho kwa upande wa wakatoliki, mafundisho ya komunio ya kwanza na kipaimara idadi yao imeshuka sana.
"Jumatatu ya pasaka tunategemea kubatiza, imekuwa ni tofauti na siku za nyuma tulikuwa tuna batiza watoto 100 lakini kwa kipindi hiki tunabatiza watoto wanane pekee,” amesema Padri Vumilia.

Kiongozi huyo wa kiroho amesema kwenye suala la ufunguaji wa ndoa vijana kutokana na changamoto ya malezi, “hawapati muda wa kijiandaa na kutafakari kuhusu kuingia katika maisha ya ndoa, hawana malezi ya kutosha ya maisha na mienendo yao."

Amesema jamii imejisahau katika taratibu na mipangilio ya malezi mtambuka.

"Imefika mahali jamii imeshindwa kujitawala kwa sababu tunaishi katika ulimwengu ambao ni huru sana, pombe zimekuwa zikipatikana katika maeneo mbalimbali, jamii ijifunze kujijengea nidhamu, wale walioaminiwa na kupewa dhamana ya uongozi katika jamii, wajifunze kutekeleza wajibu wao, kama kuna taratibu za kutoa huduma ya pombe basi zitolea katika taratibu zile ambazo zinatakiwa," amesema Padri Vumilia.


Operesheni siku 21


Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye amesema atatangaza operesheni maalumu ya siku 21 kupambana na unywaji wa pombe haramu aina ya gongo, mirungi na bangi kwa wanaokunywa pombe saa za kazi ili kuirejesha wilaya hiyo kama ilivyokuwa zamani.

Amesema maeneo mengi ya vijijini aliyopita kumekuwepo na unywaji wa pombe uliopindukia na kwamba Serikali haitakubali kuona vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa wanaangamia hivyo ataanzisha operesheni hiyo kabambe kukabiliana na hali hiyo.

"Maeneo mengi niliyoopita nimeona kuna madhara makubwa yanayotokana na ulevi wa kupindukia katika maeneo mengi ya Moshi Vijijini, kama Serikali tuna mipango kabambe ya kuhakikisha tunaweza kudhibiti vitendo vyote ambavyo vinaitoa jamii kwenye msitari," amesema Sumaye.

“Kwa hiyo kwa muda mfupi tutatangaza operesheni ya siku 21 maalumu kwa ajili ya kupambana na unywaji wa gongo, utumiaji wa mirungi na bangi na ufunguaji wa baa muda wa kazi, lengo ni kunusuru vijana wetu ambao wameingia kwenye ulevi uliopindukia, hawa vijana ni nguvu kazi yetu ya taifa.”

Mkuu huyo wa wilaya amesema, “tunataka Moshi yetu iwe ile ya zamani ya enzi na enzi ya mababu zetu, Moshi ambayo ilikuwa mstari wa mbele kwenye masuala ya elimu, tukiiacha ngazi kubwa hii ya kitaifa ikapotea maana yake tunaipeleka Moshi sehemu ambayo kwa kweli ni mbaya, hivyo kama Serikali tumejipanga.”

 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema watu wamekuwa ni walevi kupindukia na wameshindwa kufanya mambo muhimu ya kijamii na kwamba ni kama vile wanaume wamekwenda likizo.

"Watu wamekuwa ni walevi kiasi kwamba wameshindwa kufanya yale mambo ya muhimu, ndugu zangu mmejenga hii zahanati na nimeambiwa kuna chumba ambacho kinaweza kumsaidia mama kujifungua, lakini nina shaka inawezekana tukachukua watu kutokana kule Upareni kuwalatea kuja kujifungulia hapa kwasababu huku watu wameenda likizo na likizo waliyoenda ni kunywa pombe," amesema Boisafi.

"Niwaombe wale vijana wenye akili timamu, wenye umri unaofaa kwa kufuata taratibu, desturi, sheria na kanuni za kanisa wakazae watoto, hii sio amri ya mwenyeviti wa CCM Mkoa, hii ni amri ya Mungu, kwamba baada ya kufunga ndoa muende mkazae na muijaze dunia.”

Mmoja wa vijana wa kijiji hicho, Salvata Chuwa amesema vijana wenzake wengi kutokana na pombe kuwatawala wanashindwa kutongoza hata wanawake.

"Vijana sasa hivi wameishia kwenye pombe na hawataki kuoa, hawajishughulishi na kazi yoyote ile zaidi ya kulewa tu, yaani huku hakunaga wanaume wanaotongoza, wapo  wachache sana,” amesema.

Amedeus Ngawaiya, mkazi wa kijiji hicho amesema imekuwa desturi ya vijana wa maeneo hayo wanapoamka asubuhi wanawaza kunywa pombe, kuvuta bangi na kusahau majukumu muhimu ya familia.

"Ulevi umekuwa ni shida sana huku vijijini, hizi pombe zingepigwa marufuku maana vijana wetu wameisha hakuna kitu kabisa, sasa hivi wasichana wanakimbilia wazee wanasema vijana hawana nguvu, na ni kweli.

“Nina muda sijasikia harusi zikifungwa huku kwetu, ni kama vijana wameenda likizo hivi, kuna shida kubwa, kijana kumtamani msichana hakuna, mwanamke wake ni pombe," amesema Ngawaiya