Zaidi ya vijana 200, 000 kufikiwa mradi wa kudhibiti ulevi

Baadhi ya wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa Ulevi Sio Dili mjini Musoma, mradi unaotarajiwa kutekelezwa katika mikoa ya Mara na Pwani ukiwalenga vijana kudhibiti ulevi wa pombe na dawa za kulevya. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Zaidi ya vijana 220, 000 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 kutoka mikoa ya Mara na Pwani wanatarajiwa kufikiwa kupitia kampeni ya kuelimisha umma madhara ya ulevi wa kupindukia na matumizi ya dawa za kulevya.

Musoma. Zaidi ya vijana 220, 000 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 kutoka mikoa ya Mara na Pwani wanatarajiwa kufikiwa kupitia kampeni ya kuelimisha umma madhara ya ulevi wa kupindukia na matumizi ya dawa za kulevya.

Kampeni hiyo ambayo ni sehemu ya mradi wa miaka mitano wa kukabiliana na ulevi na matumizi ya dawa za kulevya wenye kaulimbiu ya “Ulevi Sio Dili’’ unaotekelezwa na shirika lilisilo la Kiserikali la ICCAO linaloshughulika na masuala ya vijana unaolenga kudhibiti wa matumizi pombe na dawa za kulevya miongoni mwa kundi la vijana. 

Akizungumza mjini Musoma leo Jumatatu Julai 2, 2023 wakati wa hafla ya kuzindua mradi huo, Msimamizi wa Mradi huo kutoka ICCAO, Maria Mrindoko amesema pamoja na vijana, mradi huo pia utawafikia na kuwanufaisha watu wazima zaidi ya 300, 000.

‘’Wilaya zitakazonufaika na mradi huu ni Musoma, Bunda na Butiama kwa mkoa wa Mara wakati kwa Mkoa wa Pwani, wilaya zitakazohusika ni Kibaha na Kisarawe,’’ amesema Mrindoko

Amesema mradi huo unawalenga zaidi vijana kutokana na takwimu kuonyesha kuwa kundi hilo ndilo ambalo ndilo nguvu kazi ya Taifa ndio linaloathiriwa zaidi na matumizi ya dawa za kulenya.

Ofisa Miradi wa ICCAO, Laurine Lyatuu amesema pamoja na kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya, mradi huo pia unalenga kupiga vita vitendo vya ukatili, unyanyasaji kijinsi na ukiukwaji wa haki unaotokana na ulevi wa pombe na matumizi ya dawa za kulevya.

"Katika kipindi hicho na hata baada ya mradi, maofisa wa ICCAO kwa kushirikiana na wenzao kutoka idara na taasisi za Serikali zinazohusiana na masuala ya ustawi wa jamii na haki jinai watapita katika vijiwe rasmi na visivyorasmi kutoa elimu kwa makundi yote kuhusu madhara ya ulevi na matumizi ya dawa za kulevya,’’ amesema Lyatuu

Amesema pamoja na sababu zingine, utafiti uliofanyika ndani ya jamii nyingi nchini unataja ulevi na matumizi ya dawa za kulevya kuwa miongoni mwa sababu za vitendo vya ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Jonas Omollo, mkazi wa Manispaa ya Musoma ameishauri Serikali kupitia mamlaka husika kushirikiana na makundi yote ya kijamii kupiga vita ulevi wa pombe wa kupindukia na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

"Zamani tulifundishwa kwamba pombe ni kwa ajili ya watu wazima ambao hata hivyo walikunywa baada ya kazi za uzalishaji shambani; lakini hivi sasa vijana wenye umri mdogo ndio wanaongoza kwa ulevi, tena nyakati za kazi,’’ amesema Omollo

Huku akiipongeza Serikali kwa kuzuia pombe za viroba vilivyokuwa vinauzwa kwa bei rahisi, Omolla ameshauri mkazo zaidi uelekezwe kwenye udhibiti wa matumizi ya ugoro, gundi, petroli na uvutaji bangi miongoni mwa vijana.