Ulimwengu: Serikali ipunguze mashangini ihudumie wazee

Mwandishi mkongwe, Jenerali Ulimwengu

Muktasari:

  • Serikali imeshauriwa kubana matumizi kwa kupunguza manunuzi ya magari ya viongozi na kuondoa misafara isiyo ya lazima ili kuelekeza fedha hizo kwenye kusaidia wazee.

Dodoma. Serikali imeshauriwa kubana matumizi kwa kupunguza manunuzi ya magari ya viongozi na kuondoa misafara isiyo ya lazima ili kuelekeza fedha hizo kwenye kusaidia wazee.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mwanaharakati ambaye pia ni mwandishi mkongwe, Jenerali Ulimwengu wakati akizungumza kwenye Siku ya Wazee iliyoandaliwa na Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bazecha), jijini Dodoma.

Ulimwengu alisisitiza fedha hizo zitasaidia kumaliza matatizo yanayowakabili wazee, ikiwemo kulipwa mafao yao ya kustaafu.

“Ninaamini kama hatua madhubuti za kudhibiti matumizi zikichukuliwa, naona tutafanikiwa kuokoa fedha nyingi zitakazotumika kuwalipa wazee pensheni,” alisema Ulimwengu.

Hivi karibuni akiwa bungeni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali itabana matumizi kwa kupunguza mambo mbalimbali

Hoja hiyo ilitokana na malalamiko ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya kielektroniki, hivyo Waziri alisema watakata fedha za chai na vitafunwa kufidia mapato hayo.

Alisema watapunguza misafara ya ndani na nje ya nchi kwa maofisa wa wizara na kupunguza mafunzo, semina, warsha na matamasha.

Aidha, alisema fedha hizo pia zitakatwa kwenye makundi ya viongozi wanaokwenda kukagua mradi uleule kwa nyakati tofauti au makundi yanayokwenda eneo lilelile kila mtu na gari lake.

Awali, Ulimwengu aliwaomba vijana kuangalia changamoto zinazowakabili wazee kwa kujiepusha nazo mapema, kwani vijana wengi sasa wamejiingiza kwenye michezo ya kamari badala ya kufanya kazi kwa bidii.

Alisema sasa kumeibuka tabia ya vijana wengi kubweteka, hasa kwenye vyama vya siasa kwa viongozi kuwavika vyeo vya ukamanda wa vijana.

Pia alisema Serikali inatakiwa kulinda maslahi ya wazee na kuimarisha jamii yenye haki, ustawi na kuondoa chuki, ulaghai na ukandamizaji.

Naye Mwenyekiti wa Bazecha, Juma Issa, aliiomba Serikali kuandaa Baraza la wazee litakalosimamia na kumshauri Rais, Mahakama na wabunge.

Alisema Serikali iunde wizara itakayoshughulika na wazee kwa kupunguza changamoto zao kwa kuwawekea utaratibu wa kuwalipa pensheni kila mwezi.