Umeme wa gridi ya Taifa GGML kuwashwa Machi 2023

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kinu cha kupoza umeme kinachojengwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) lengo ni kuiwezesha kampuni hiyo kutumia umeme kutoka gridi ya Taifa.

Geita. Serikali ya Tanzania imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kinu cha kupoza umeme kinachojengwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) lengo ni kuiwezesha kampuni hiyo kutumia umeme kutoka gridi ya Taifa.

Kuanza kwa kampuni hiyo kutumia umeme wa gridi ya Taifa, utaiwezesha kuachana na uzalishaji wa nishati hiyo ya umeme wa mafuta ambao una gharama kubwa.

Kinu hicho kitakuwa na uwezo wa kupitisha umeme wenye kilovolt 13 kwenye mitambo yake ambapo hadi kikamilike kinatarajiwa kugharimu Sh50 bilioni huku Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) nalo linajenga njia ya kupeleka umeme katika mgodi huo yenye urefu wa kilomita sita.


Hayo yalisemwa na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko mara baada ya kufanya ziara katika Mgodi wa GGML uliopo Geita ambapo alisema anaamini kufikia Machi 2023, kamouni hiyo itaanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa.

“GGML wanataka kuhama kutoka kwenye matumizi ya umeme unaozalishwa kwa mafuta kwenda umeme wa Tanesco, kupitia substation inayojengwa kwa dola za Kimarekani milioni 20.

“…wamekwenda kwenye hatua nzuri, naamini mpaka itakapofika Machi mwakani tutawasha umeme wa Tanesco kuendesha mgodi wetu hapa ndani na utapunguza gharama ambazo sasa zinatumika,” alisema Dk Biteko.

Kwa upande wake, Makamu Rais wa kampuni ya AngloGold Ashanti inayomiliki Geita Gold Mining Limited (GGML), Simon Shayo alisema kukamilika kwa mradi huo, kutapunguza gharama za uendeshaji wa mgodi na uzalishaji wa umeme kwa asilimia zaidi ya 50.

Alisema mgodi wa GGML unatumia zaidi ya megawati 40 zinazozalishwa kwa kutumia jenereta zinazotumia mafuta ya dizeli tangu mwaka 2018, hali inayoongeza gharama kubwa za uendeshaji.

“Sasa tupo kwenye mchakato wa kujenga kinu cha kupoozea umeme chenye thamani ya karibu Sh50 bilioni na Tanesco watajenga njia ya kilomita sita kufikia hapa kwenye mgodi wetu,” alisema na kuongeza:

“Kwa kasi hii tunayokwenda nayo sisi na wenzetu wa Tanesco hadi kufikia Machi 2023, tutakuwa tumeingia kwenye umeme wa gridi ya Taifa na tutakuwa tumepunguza gharama yetu ya umeme kufikia asilimia 50, kutoka uniti moja kwa senti 19 kwenda unit moja kwa senti tisa (US $),” alisema.

Alisema kukamilika kwa mradi huo wa kupeleka umeme kwenye Kampuni ya GGML kunatarajiwa kutaiwezesha Tanesco kupata Sh5 bilioni kwa mwezi zitakazotokana na mauzo ya umeme.