Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umemuandaaje mtoto kusherehekea Krismasi?

Kesho ni Desemba 25, 2023, siku ambayo Wakristo duniani kote wanasherehekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo.

Ni utamaduni wa jamii nyingi, wakiwamo Watanzania inapofika kipindi cha sikukuu hiyo huwa na namna wanavyosherehekea na kuifurahia.

Familia nyingi, wakiwamo watoto hujumuika pamoja kwa kusherehekea kwa kula, kunywa na kucheza ili kuadhimisha siku hii kwa furaha.

Licha ya kujumuika pamoja, wapo wanaosafiri mbali na makazi yao na wengine hubadilisha mandhari ya nyumba wanazokaa ili kuwa na mwonekano wa tofauti katika siku hiyo muhimu.

Ni wazi kuwa, katika kusherehekea sikukuu ni ngumu kuwasahau watoto katika suala zima la mitindo na namna gani wanatakiwa kuvaa ili kuwawezesha kusherehekea kwa furaha.

Kila mzazi au mlezi hutamani kumuandaa mtoto wake kwa mitindo tofauti ya mavazi au nywele, lengo likiwa ni kufikisha upendo kwa mtoto husika.

Kuna mambo muhimu ambayo wazazi na walezi wanapaswa kuzingatia kwa watoto wao ili kuwapa mwonekano wa kipekee na uhuru wa kusherehekea sikukuu.
Kwa mujibu wa mtandao wa mightykidsacademy.com, hali ya hewa ni kitu kikubwa kwa mzazi kufanya uamuzi ni nguo ya aina gani atachagua kwa ajili ya kumvalisha mtoto.

Kama ni kipindi cha joto mtoto avalishwe nguo aina ya pamba zinazompa hewa na kama kipindi cha baridi avae nguo zilizotengezwa kukabiliana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao huo, kama unanunua nguo kwa ajili ya mtoto hakikisha inamtosha ili kumuepusha na usumbufu utakaomnyima raha pindi anapoivaa.

Mtoto Happyness Mambwe anasema sikukuu iliyopita, mama yake alimnunulia nguo inayombana kwa sababu aliipenda, akavaa hivyo hivyo.
Happyness anasema alikosa uhuru na aliamua kuivua.
 

Nguo watakazovaa sikukuu

Akizungumza na Mwananchi, Mama Nancy anasema katika suala la kuwachagulia watoto nguo huzingatia kimo na umbo la watoto wake.

Anasema huwa anachukia akiona mtoto amevalishwa nguo isiyo ya kimo chake hadi anaamua kuishikilia ili aweze kutembea vizuri, kitu ambacho sio sahihi kwa mtoto.

"Mtoto sio kama mtu mzima ambaye anajua kipi kinafaa na kipi hakifai, yeye akiona nguo mpya tu akili inamtuma kutamani kuivaa.

“Lakini unaikuta nguo hiyo kubwa na wakati mwingine inambana mpaka anashindwa kupumua vizuri au anatembea ameishikilia, inamkosesha amani, "anasema mama Nancy.

Mzazi mwingine, Fransisca John anasema amemuandaa vyema mtoto wake kwa kamnunulia nguo ambayo haitampa usumbufu.

“Unajua watoto wanakua vimo, tofauti na sisi watu wazima, kwa hiyo huwa nahakikisha nawanunulia wanangu nguo ambazo sio kubwa na wala haziwabani, yaani size yao kabisa,” anasema Fransisca, mama wa watoto wawili.

Kauli ya Fransisca inashabihiana na ya Glory Michael, anayesema akiwa dukani katika kununua nguo, anajua mtoto wake ni nguo ya aina gani inamtosha.
“Hata ninapofika nyumbani lazima nimjaribishe, nikiona haimtoshi huwa nairudisha, siwezi kumnyima raha mwanangu kwa kitu kisichomtosha,” anasema Glory.
 

Viatu kulingana na mazingira

Viatu vya kuvaa watoto katika matembezi ya sikukuu vinapaswa kutokuwa na kisigino kirefu ili kuwapa urahisi wa kutembea na kuzingatia uimara wa kiatu kuepuka kukatika.

Mazingira kama sehemu za fukwe huko kuna mchanga ambao huleta shida endapo mtoto akiwa amevaa viatu virefu au vinavyoteleza.

Faith Kimario anasema haoni haja ya wazazi kuwanunulia watoto viatu vinavyowawia ugumu kuvaa, kuna wakati mtoto anavishwa viatu vimembana hadi anashindwa kutembea, sikukuu inageuka adhabu kwake.

"Baadhi ya wazazi huwavisha watoto viatu vyenye kisigino kirefu au vikiwa vimewabana, hali inayowanyima uhuru watoto wanaposherehekea sikukuu, mtoto anatakiwa afurahie na sio kuteseka na fasheni,” anasema Faith.
 

Mitindo ya nywele

Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wa afya, ngozi ya kichwa ya mtoto haijakomaa, hivyo misuko inayotakiwa iwe rafiki isiyompa maumivu na karaha.

Kwa watoto wa kiume kama wananyoa mzazi ahakikishe mtoto hanyoi mtindo unaohatarisha maadili ya mtoto kama kiduku, hali inayoweza kumkosesha raha kwa baadhi ya watoto wenzake wakianza kumshangaa na wakati mwingine kumdhihaki.

Akizungumza na Mwananchi, Emmanuel Lyaunga anasema siku hizi mitindo ya nywele kwa watoto wa kike imekuwa kama sehemu ya ukatili.

Lyaunga anasema watoto wamekuwa wakisukwa nywele ambazo huwaletea maumivu na wakati mwingine kupoteza haiba ya utoto.

“Pia watoto wa kiume wananyolewa hovyo na kuwekwa dawa kichwani ambazo huwa zina kemikali, hivyo kuwaathiri afya taratibu,” anasema Lyaunga.

Mfanyakazi wa saluni aliyejitambulisha kwa jina Aunt Sammy anasema huwa wanawashauri wazazi wasiwachagulie watoto misuko ya kiutu uzima kwa kuwa inawaumiza.

“Lakini kuna wazazi wakali, wanachokitaka ndio hicho hicho, matokeo yake unamsuka mtoto huku analia,” anasema msusi huyo wa eneo la Kariakoo.
 

Sehemu za matembezi

Kuna maeneo kama ya fukwe, siku za sikukuu sehemu hizi huwa zinakuwa na wingi wa watu.

Kama ambavyo Jeshi la Polisi linatahadharisha mara kwa mara, kama unahitaji kwenda kutembea na familia unapaswa uwe makini, hasa kwa watoto kuepuka majanga kama ya kuzama wakati wa kuogelea na kupotea kutokana na msongamano wa watu.

Akizungumza na Mwananchi, Innocent Focus anasema katika siku za sikukuu wazazi na walezi wanapaswa kuwa makini kwa kuchagua sehemu salama za kwenda kutembea ili kuepuka hatari. Anasema siku za sikukuu wahalifu huzitumia vyema kujipatia kipato kwa njia isiyo halali.

Baada ya shamrashamra za Krismasi, siku inayofuata ni maalumu kwa ajili ya kufungua zawadi. Siku hii inafahamika zaidi kama ‘boxing day’ na huadhimishwa kila Desemba 26’ ikiwa ni siku moja baada ya sikukuu ya Krismasi.
 

Boxing day

Historia ya siku hii ilianzia nchini Uingereza, ambako ilikuwa siku maalumu ya watu wenye uwezo kutoa zawadi kwa maskini au wafanyakazi wasio na uwezo.

Wapo wanaoona kuwa utaratibu huu unawahusu watu wenye uwezo au wasomi, lakini ukweli ni kwamba zawadi inaweza kutolewa na mtu yeyote.

Kama inavyofahamika hakuna asiyependa kupewa zawadi, kibinadamu wote tumeumbwa kupenda kupokea zawadi bila kujali ukubwa au thamani yake.