Unachopaswa kujua kuhusu chakula kilichoongezwa virutubishi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Kuna aina kadhaa zinazoweza kutumika kuongeza virutubisho ikiwamo kupitia mashine za kusaga viwandani na hata kuongeza wakati wa kula.

Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema mchele ulioongezwa virutubishi, maharage na mafuta ya kupikia vilivyotolewa msaada na Wizara ya Kilimo ya Marekani,  ni salama kwa matumizi ya binadamu.

TBS katika taarifa kwa umma iliyotolewa Jumapili Machi 17, 2024, iliyosainiwa na Meneja Uhusiano na Masoko wa shirika hilo, Gladness Kaseka imesema:

“TBS inapenda kuujulisha umma kuwa chakula hicho kilifuata taratibu za uingizwaji wa chakula nchini, kilipofika kilifanyiwa ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa matumizi.”

Pia imesema utaratibu wa kuongeza virutubishi kwenye chakula, unakubalika kitaalamu na hufanyika kwa lengo la kuboresha hali ya lishe kwa walaji.

TBS imetoa taarifa hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kueleza Tanzania inazalisha mchele na maharage kwa kiwango cha kutosha, hivyo Marekani wanunue vyakula hivyo nchini na kuviongeza virutubishi ndipo watoe msaada.

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Ijumaa Machi 15, 2024 kupitia mtandao wa X (zamani twitter) uliweka picha iliyoonyesha viroba vya mchele, vikiambatana na ujumbe uliosomeka:

"Chini ya mpango wa 'Pamoja Tuwalishe', Wizara ya Kilimo ya Marekani, kwa ushirikiano na jumuiya za kimataifa, imetoa msaada wa kwanza wa mchele ulioongezwa virutubishi, maharage na mafuta ya alizeti kutoka kwa wakulima wa Marekani moja kwa moja hadi shuleni katika eneo la Dodoma nchini Tanzania."

Ujumbe huo ulieleza msaada huo unalenga zaidi kutoa milo yenye lishe kwa wanafunzi wa shule zaidi ya 300 zinazoshiriki; ukieleza mbali na mchele, pia wataanzisha bustani za shule na kufunza mbinu za kuvuna.

Loading...

Loading...


Virutubishi ni nini?

Ofisa Lishe Manispaa ya Kinondoni, Janeth Mnzava amesema virutubishi vinaweza kuwa madini, vitamini au asili ya protini vinavyoongezwa ambavyo ama havipo kwa wingi katika chakula husika au havipo kabisa kwenye vyakula vingine.

Amesema huongezwa kwenye chakula kwa lengo la kuhakikisha mtu anapata mahitaji yake ya kila siku kulingana na namna anavyopungukiwa na aina hiyo ya kirutubishi.

Janeth amesema kuna aina mbalimbali ambazo zinaweza kutumika kuongeza virutubishi kupitia mashine za kusaga, viwandani lakini pia unaweza ukaongeza wakati wa kula.

“Unaweka kiwango kwa mlo wa mtu mmoja na kuna aina mbalimbali za vyakula vilivyoongezwa virutubishi vya madini, vitamini na hii tunaona kwenye maziwa au siagi, unga wa mahindi, unga wa ngano na mafuta wanaongeza vitamini A au B,” amesema.

Janeth ameongeza: “Kuna vyakula vyenye asili ya mafuta pia wanaongeza Omega 3, mafuta ya samaki yale wanaongeza kwa ajili ya kuboresha afya ya moyo na ubongo, kuna vyakula vya nyuzi-nyuzi wanaongeza pia virutubishi. Kwa ujumla vyakula vinaongezwa virutubishi kwa kuwa ni njia ya ziada ya kupata virutubishi muhimu kwa ajili ya afya ya makuzi ya mwili.”


WHO na virutubishi kwenye mchele

Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia tovuti yake, limependekeza virutubishi vya vitamini A kwenye mchele kama moja ya mkakati wa afya ya umma ili kuboresha madini chuma na lishe ya vitamini A kwa watu. Pia, linapendekeza virutubishi vya asidi ya foliki.


Wadau wa lishe wafafanua

Akizungumzia suala hilo, Meneja Mradi wa Vyakula vinavyoongezwa virutubishi kibaiolojia wa Taasisi ya Gain Tanzania, Josiah Edwin, amesema kuongeza virutubishi kwenye chakula si jambo la ajabu kwa sababu hadi sasa Tanzania ina vyakula vya aina nne ambavyo ni lazima vifanyiwe hivyo.

“Tanzania tuna aina nne ya vyakula ambavyo ni mandatory (lazima) viongezwe virutubishi ambavyo ni chumvi, mafuta ya kula, unga wa mahindi na unga wa ngano,” amesema.

Edwin amesema mchele kuongezewa virutubishi haikatazwi bali si lazima  na kama unatokea nje ya nchi, TBS inakuwa na jukumu la kupima usalama wa chakula husika.

“Virutubishi vinasaidia kupunguza magonjwa ya utapiamlo katika jamii, mfano goita, kichwa kikubwa, mgongo wazi na mdomo wa sungura kwa kuongeza baadhi ya madini katika chakula ikiwamo foliki asidi,” amesema.

Kuhusu mchele ulioongezwa virutubishi kutokea Marekani, Edwin amesema teknolojia ya kuongeza virutubishi kwenye mchele ni ngumu, na kwa sasa Tanzania haipo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Oktoba 26, 2023 akizindua mashine ambazo zitatumika kuongeza virutubishi kwenye unga wa nafaka unaozalishwa na wasindikaji wadogo nchini. Picha na Maktaba

TFNC yaeleza hali ilivyo

Februari 22, 2024 Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk Germana Leyna alisema inakadiriwa asilimia 70 hadi 90 ya vyakula vinavyosindikwa nchini katika viwanda vikubwa vinaongezwa virutubishi hususani unga wa ngano, mafuta ya kula na chumvi.

Dk Leyna alisema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha 37 cha Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula nchini, kilichofanyika mkoani Morogoro.

“Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutambua njia bora za kukuza ushiriki wa sekta binafsi katika afua za uongezwaji wa virutubishi kwenye vyakula ili kupambana na changamoto za utapiamlo wa kupungukiwa vitamini na madini,” alisema Dk Leyna.

Alisema juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha asilimia kubwa ya unga wa mahindi unaongezwa virutubishi vya vitamini na madini na tayari mpaka sasa zaidi ya vifaa 1,026 vya kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi vimeshafungwa na Shirika la SANKU kwenye mikoa 26 nchini.

Hali ya udumavu

Ripoti ya TDHS-MIS ya mwaka 2022 ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),  imeonyesha hali ya udumavu nchini imepungua kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 30 mwaka 2022.

Hata hivyo, bado kuna mikoa inaongoza kwa hali hiyo ikiwamo Iringa na Njombe.

Mikoa 10 yenye kiwango kikubwa cha udumavu nchini kwa mujibu wa ripoti hiyo ni Iringa (asilimia 56.9), Njombe (asilimia 50.4), Rukwa (asilimia 49.8), na Geita (asilimia 38.6).

Mingine ni Ruvuma (asilimia 35.6), Kagera (asilimia 34.3), Simiyu (asilimia 33.2), Tabora (asilimia 33.1), Katavi (asilimia 32.2), na Manyara (asilimia 32).

Kiwango cha udumavu kwa Mkoa wa Dodoma ripoti hiyo inautaja kuwa na asilimia 31.


Mkakati wa Serikali

Oktoba, 2023 mkoani Arusha ilielezwa katika kukabiliana na tatizo la udumavu, Serikali inatarajia kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa mashine maalumu ya kuchanganya virutubishi kwenye vyakula.

Uzinduzi wa mashine ya kwanza kutengenezwa nchini ulifanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea mabanda ya maonyesho kabla ya kufunga mkutano mkuu wa tisa wa wadau wa lishe nchini, katika hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.

Mashine hiyo inachanganya virutubishi vya Vitamini B, foliki asidi, madini ya chuma na zinki kwenye mahindi wakati wa kusaga.

Foliki asidi ni muhimu kwa ukuaji wa ubongo na uti wa mgongo kwa watoto wanaotarajia kuzaliwa. Matumizi yake sahihi husaidia kuzuia tatizo la mgongo wazi na vichwa vikubwa kwa watoto.

Waziri Mkuu Majaliwa alizindua mashine hizo Oktoba 26, 2023 ambazo zitatumika kuongeza virutubisho kwenye unga wa nafaka unaozalishwa na wasindikaji wadogo nchini.

Mashine hizo zimetengezwa nchini na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) chini ya ufadhili wa Gain Tanzania kupitia uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu). Zitasaidia kuendeleza juhudi za pamoja za wadau wa lishe katika kuhakikisha Tanzania inapunguza viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, alisema kwa kipindi kirefu nchi imekuwa ikikabiliana na changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kuchanganyia virutubisho kwenye vyakula vyenye bei nafuu.

“Serikali imepata mafanikio makubwa kupitia Sido na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), kwa kushirikiana na Shirika la Gain ambalo limewezesha kukamilika kwa kazi hiyo na kuwa wa kwanza kununua na kusambaza mashine hizo katika maeneo tofauti yenye wazalishaji wadogo ambao ndiyo kundi kubwa linalolisha wananchi wengi,” alisema Jenista.

Meneja mradi wa urutubishaji vyakula kutoka Gain Tanzania, Archard Ngemela, alisema mashine za mwanzo 50 zitatolewa kwa mikoa ya Kagera, Iringa, Mara, Manyara na Kilimanjaro, kila mmoja ukipatiwa 10. Mikoa hiyo ipo katika eneo la mradi wa Gain wa urutubishaji chakula.

Alisema mashine zimetolewa kupitia ushirika wa wasindikaji wa mahindi ulioundwa kwa kila mikoa ya mradi chini ya usimamizi wa Gain.