Wazabuni watakiwa kuongeza virutubisho vyakula vya shule

Muktasari:

  • Wazabuni wanaosambaza vyakula katika shule mbalimbali Moshi wametakiwa kuhakikisha wanaongeza virutubisho katika vyakula hivyo ili wanafunzi wawe na afya bora.

Moshi. Serikali Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro imewataka wazabuni wanaosambaza vyakula shuleni waongeze virutubisho katika vyakula hivyo kwa ajili ya lishe ya wanafunzi.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Mei 17, 2023 na Afisa lishe wa Manispaa hiyo, Hadija Kitumpa wakati wa kikao cha kamati ya Lishe ambapo amesema wazabuni wanaosambaza vyakula mashuleni, wanapaswa kuzingatia mwongozo wa chakula na lishe kikamilifu ili kusaidia wanafunzi kupata kinga zaidi na kuimarisha afya zao.

Amesema vyakula vinavyotakiwa kuongezewa virutubisho ni pamoja na mahindi na chumvi ambayo huongezwa madini joto, ambapo virutubisho hivyo husaidia kuimarisha kinga za mwili na kuboresha afya.

"Tunapozungumzia virutubisho kuna vile vyakula vimeongezwa virutubisho vikiwa shambani, lakini kuna vile vyakula ambavyo vimeshazalishwa, sisi tunaongeza virutubishi, mfano mahindi ya njano yalishaongezwa virutibisho kama mbegu kabla ya kupandwa, lakini mahindi meupe yanakuwa yana virutubishi vya kawaida hivyo tunayaongezea.

"Virutubisho ambavyo vinaongezwa kwenye unga wakati wa kusaga ni madini ya Zink, madini ya Folic, madini ya chuma na vitamini B12, lengo kubwa pia ni kuimarisha via vya uzazi kwa watoto wetu ambao wanazaliwa na wale balehe inawasaidia katika kipindi hicho,”amesema.

Kwa upande wake Afisa Kilimo Manispaa ya Moshi, Martha Kimambo aliyehudhuria kikao hiko amesema tayari wametoa elimu kwa wananchi 353 kuhusu kanuni bora za kilimo ili kuboresha lishe kwa jamii hasa katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo.

“Lakini pia tumetoa elimu kwa wakulima 139, juu ya uhifadhi wa chakula ili kulinda usalama wa chakula katika ngazi ya kaya,”amesema.