Unajua kiasi cha maji unachopaswa kunywa kwa siku?

Muktasari:

  • Maji husaidia figo husawazisha shinikizo la damu, kusafisha na kutoa kiasi cha chumvi kilichozidi mwilini, kuondoa taka mwili ikiwemo urea na uchafu mwingine kupitia mkojo.

Dar es Salaam. Unakunywa maji kiasi gani kwa siku? Kama ulikuwa hujui wataalamu wa afya wanashauri ili figo zako ziendelee kuwa imara unapaswa kunywa maji lita moja kwa kila kilo 25 za mwili wako.

Hii inamaanisha kuwa kama uzito wako ni kilo 50 utapaswa kunywa maji lita mbili  kwa siku na iwapo kilo zako ni 75, lita tatu zinakufaa kwa saa 24.

Kwa mujibu wa wataalamu, unywaji mwingi wa maji huzuia mawe kwenye figo, husafisha madini ya sodiamu na urea na inashauriwa kunywa kiasi hicho ili kufikia kiasi cha mkojo cha angalau lita 2.0 hadi 2.5 kwa siku ili kuzuia maradhi katika figo.


Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Januari 8, 2024 na Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige alipokuwa akielezea changamoto za kuongezeka kwa wagonjwa wa figo nchini na magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema iwapo mtu ana uzito wa kilogramu 62 anapaswa kunywa maji lita 2.53 ambayo ni sawasawa na vikombe vya chai sita mpaka vinane.

“Kwa kunywa hivyo unajaribu kuokoa figo zako, unajaribu kuweka mwili wako katika hali nzuri na unajaribu kuimarisha afya yako kwa sababu asilimia 60 ya uzito wako ni maji, kwahiyo kila kitu mwilini kina namna yake ya kujiendesha,” amesema.

Dk Mzige ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa kinga Wizara ya Afya mwaka 2005, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kliniki ya Mshangai iliyopo Korogwe mkoani Tanga, amesema changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza kwa sasa yanapaswa kutatuliwa kwa kinga badala ya kusubiri watu waugue.

“Ulaya wanabadilisha mtindo wa kutibu wagonjwa, kwa sasa hawatumii dawa lakini wanatumia chakula, mazoezi na vitu vingine ikiwemo usingizi, kwa hiyo ni vitu ambavyo vinahitajiwa kufanyiwa kazi,” amesema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo ambaye amesema tabia ya kutokunywa maji ya kutosha, husababisha uzito uliokithiri kwa mujibu wa utafiti uliofanywa jijini Dar es Salaam.

Dk Pedro ambaye amewahi kufanya tafiti nyingi amesema wakazi wa Jiji la Dar es Salaam hawazingatii mlo kamili, hula vyakula vilivyopikwa kwenye mafuta mengi, vilivyosindikwa na bila kuzingatia wakati sahihi wa kula na hawana utamaduni wa kunywa maji ya kutosha.

“Mwaka 2020 JKCI tumewahi kufanya utafiti ambao ulionyesha asilimia 67.2 ya wakazi wa jijn hilo wana uzito kupita kiasi, huku idadi kubwa ya watu hao ikionekana ni wanywaji wa pombe wa mara kwa mara na hawanywi maji ya kutosha,” amesema.

Amesema utafiti huo uliangalia aina ya ulaji wa watu, ufanyaji wa mazoezi, unywaji wa maji na uvutaji wa sigara.

“Hali hii inachangia shinikizo la juu la damu, wanywaji wa pombe na watu wasiozingatia unywaji wa maji, tabia bwete na kutoushughulisha mwili walau nusu saa kwa siku tano za wiki ndiyo wanaoathirika zaidi na uzito uliopitiliza,” amesema Dk Pedro.

Maji husaidia kazi mbalimbali mwilini kama vile mmeng'enyo wa chakula, mwili kuwa angavu (kutokua mkavu), kusawazisha ujazo wa damu mwilini, kusaidia figo katika shughuli zake ikiwemo kusafisha na kutoa kiasi cha chumvi kilichozidi mwilini, urea na uchafu mwingine kupitia mkojo na mengineyo.


Kwa mujibu wa mtandao wa Dailymail, unywaji wa maji ya kutosha unaweza kupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo.

“Utafiti uliofanywa Marekani kwa muda wa miaka sita umeonyesha kuwa watu wanaokunywa glasi za maji zisizopungua tano kila siku, hujiepusha na uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa moyo kwa asilimia 41 zaidi ya wale wanaokunywa glasi mbili  au chini ya hapo,” imeeleza taarifa hiyo.

Imeelezwa kuwa utaepushwa na saratani ya tumbo kwa kunywa maji, kwani maji husaidia usagaji wa chakula tumboni na hivyo wakati wote tumbo lako litakuwa safi na hivyo kujiondoa katika hatari ya kupata saratani ya tumbo kwa asilimia 45 na 50 kwa saratani ya kibofu cha mkojo.