Unywaji sahihi wa maji hulinda afya ya mwili

Muktasari:

  • Jana umekunywa kiwango gani cha maji? Leo je, hadi muda huu unasoma makala hii umeshakunywa kiwango gani cha maji? Nadhani, tutakubaliana kuwa wengi wetu huwa hatuzingatii sana suala la kunywa maji. Hii inatokana na wengi hatujui umuhimu wa kunywa maji.

Jana umekunywa kiwango gani cha maji? Leo je, hadi muda huu unasoma makala hii umeshakunywa kiwango gani cha maji? Nadhani, tutakubaliana kuwa wengi wetu huwa hatuzingatii sana suala la kunywa maji. Hii inatokana na wengi hatujui umuhimu wa kunywa maji.

Jambo ambalo najua pengine wengine litawashtua ni kwamba asilimia 60 ya mwili wa binadamu ni maji. Ndiyo, ni maji. Hivyo inamaanisha yana umuhimu kwa maisha na uhai wetu. Umuhimu huu unatokana na nini lakini?

Tuanzie kwanza kwenye uchafu wote ulio ndani ya mwili na unaotengenezwa ndani, ikiwemo sumu zinazotolewa nje ya mwili kwa njia ya maji. Hapa ndipo figo inahusika sana, maana figo hufanya kazi ya kuwa chujio la uchafu, lakini ili figo iweze kufanya kazi hii vizuri ni lazima unywe maji, maana kazi ya kusafirisha uchafu huo kwenda nje ya mwili kwa njia ya mkojo inafanywa na maji. Sasa basi, nini kinatokea kama hunywi maji ya kutosha? Uchafu mwingi utashindwa kutolewa kwenye figo na uchafu unaofanikiwa kutolewa utatolewa kwa shida sana. Hapa ndipo tunaanza kupata changamoto za kiafya kama vile mawe kwenye figo.

Mnisamehe kwa kuuliza, hivi rangi ya mkojo wako ikoje, ni rangi ya njano iliyokolea sana au wastani au inaelekea kuwa kama mweupe? Kama ulikuwa huangalii rangi ya mkojo wako basi ni muhimu sana uanze leo, maana rangi ya mkojo inaweza kukupa ishara moja kwa moja kama unakunywa maji ya kutosha au la.

Ipo hivi, ukiwa unakojoa mkojo ambao sio mzuri kwa sababu mchujo wa uchafu kwenye figo haukufanyika vizuri, basi ile mirija ya kuusafirisha kutoka kwenye figo kwenda nje inaziba au kwenye njia kunakuwa na vimawe mawe vidogo kama mfano wa chumvi chumvi.

Hali hiyo ikiendelea kwa muda mrefu unajikuta unatengeneza magonjwa makubwa ambayo ungeweza kujiepusha. Hali hii pia inaweza kuchangia sana kupata maambukizi ya njia ya mkojo, kama vile ugonjwa wa UTI na kujirudia mara kwa mara.

Tukija kwenye damu, asilimia 80 ya damu ni maji, hivyo yana kazi muhimu ya kusafirisha vitu ambavyo vipo kwenye damu. Usipokunywa maji ya kutosha, kiwango cha kemikali kwenye damu kinakuwa kikubwa na damu inakuwa nzito, hivyo kupelekea changamoto wakati wa kusafirishwa kwenye mishipa midogo. Hii inaweza kufanya mishipa ya damu midogo ikaziba na kuleta matatizo makubwa ya kiafya.

Madaktari wanatuambia kuwa mtu mwenye uzito wa kilo 7 anapaswa anywe maji lita 3 kwa siku. Kama una uzito huo na unakunywa maji chini ya hapo basi yakupasa kuongeza jitihada. Hii inamaanisha kwa wastani wa kila kilo 23 basi unywe lita moja ya maji.

Tukubaliane kila mmoja wetu kunywa maji zaidi ya kiwango cha sasa halafu tuangalie namna ambavyo mwili unaanza kujisikia, kuanzia uchovu hadi rangi ya mkojo. Lakini soda, juisi, chai, pombe siyo maji, hivyo tunaposema tunywe maji inamaanisha maji na si kimiminika kingine.

Neema Lugangira ni mbunge wa viti maalumu kupitia kundi la NGO’s, pia ni mtaalamu wa masuala ya lishe, wasiliana naye kwa: Instagram/Twitter/Facebook: @neemalugangira