Upelelezi kesi ya Muharami, wenzake wakamilika, kusikilizwa Januari 16

Muktasari:

  • Muharami Sultan na wenzake wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za Kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 34.89.

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 34.89 inayomkabili aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba Sport Club, Muharami Sultan (40) na wenzake watano, umekamilika.

Tayari Serikali imeshapeleka nyaraka muhimu za kesi hiyo Mahakama Kuu kwa ajili ya kusajiliwa na kisha washtakiwa hao watasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo kabla ya kuhamishwa Mahakama ya juu.

Wakili wa Serikali, Caroline Matemu ameieleza Mahakama ya Hakimu ya Hakimu Mkazi, leo Januari 2, 2023, wakati kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 71/2022 ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Matemu ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Sultani na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 34.89.

Wakili Matemu amedai upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuja kuwasomewa washtakiwa idadi ya mashahidi na vielelezo
Hakimu Mrio, baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 16, 2023 itakapotajwa na washtakiwa wapo rumande kutokana na kesi inayowakabili haina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kesi hiyo imeendeshwa kwa njia ya video, huku washtakiwa wakionekana kwenye video kupitia runinga iliyowekwa katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama ya Kisutu.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo Novemba 21, 2022 wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya.

Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif; Said Matwiko, mkazi Magole; Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54), mkazi wa kisemvule; John John maarufu  ‘Chipanda’ (40), mkazi wa Kitunda na Sarah Joseph.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa Oktoba 27,2022 eneo la Kivule jijini Dar es Salaam kwa pamoja walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 27.10.

Pia, Novemba 4, 2022 maeneo ya Kamegele wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani washtakiwa kwa pamoja walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 7.79.