Usafiri Barabara ya Morogoro hali  tete, eneo la Jangwani lafungwa 

Muktasari:

  • Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimesababisha Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani  kufungwa na kuzuia magari kuingia katikati ya jiji 

Dar es Salaam. Abiria na watu wenye magari wanaotumia Barabara ya Morogoro wameshindwa kuendelea na safari baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini hapa kujaza maji eneo la Jangwani  na kusababisha barabara hiyo kufungwa. 


Mvua hizo zilizoanza kunyesha leo Januari 20 2024 saa kumi alfajiri  kwa kuambatana na upepo mkali zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali jijini. 


Mkazi wa Kimara, Aisha Salehe ameieleza Mwananchi Digital kuwa wamepanda basi la mwendo kasi Kimara lakini walipofika Jangwani waliambiwa na dereva kuwa gari hilo haliwezi kwenda Kariakoo kutokana na mafuriko yaliyopo.


Amesema alipanga gari hilo saa 11: 30 asubuhi ili li aelekee kwenye biashara zake anazofanya eneo la Kariakoo lakini ameshinda kwenda kutokana na usafiri huo kuishia hapo.


"Nipo hapa Jangwani nasubiria maji yapungue kidogo ili niende kariakoo kwa ajili ya kufanya biashara, nategemewa niuze nguo ili familia yangu iweze kula na maisha yasonge mbele," amesema Aisha.


Mkazi wa Mbezi, Raphael Ismail amesema usafiri umekuwa wa shida kutokana magari ya mwendo kasi kuishia Magomeni hali iliyomlazimu aingie hasara ya kuchukua bodaboda kwa Sh15,000 ili apelekwe Kariakoo kupitia Ilala Boma.


Kwa magari ya daladala yanayofanya safari Mabibo kwenda Kariakoo na Makumbusho zinazoelekea Posta nayo sasa yanaishia Magomeni  kutokana na Jangwani kutopitika.


Mkazi wa Mabibo, Hemed Rashid amesema ametoa nauli ya Sh600 kuelekea Kariakoo, lakini walipofika Magomeni wakaelezwa na dereva kuwa wao wanaishia Magomeni kutokana na maji kujaa Jangwani.


Rashid amesema yeye baada ya kushuka wameungana na wenzake watano ili waweze kuvuka kwenye maji yaliyopo Jangwani.


"Usafiri ni mgumu ukisema upitie Boma unaweza kufika Kariakoo saa tisa alasiri kutokana na foleni iliyopo, hivyo tumefanya uamuzi wa kuvuka kwa pamoja Ili tuweze kuwahi kwenye biashara zetu," amesema Rashid.


Hata hivyo,  ameiomba Serikali itengeneza barabara za juu waachane na magari ambayo yapo pale Jangwni yanayotoa mchanga kwa kuwa hayasaidii mvua zinaponyesha maji yanapita juu ya daraja la Jangwani.


Dereva wa Makumbusho, Issa Salehe amesema wanalazimika kuishia eneo la Magomeni kutokana barabara ya Jangwani haipitiki na hawezi kupita Boma kutokana na foleni iliyopo eneo hilo.