Usajili wa ndege zisizo na rubani sasa ndani ya siku 14

Dar es Salaam. Warusha ndege zisizokuwa na rubani (drones) 245 wamesajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ili watumie vifaa vyao katika maeneo tofauti nchini, tangu utaratibu huo uanze mwaka 2020.

Hayo yameelezwa juzi jijini hapa katika uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya usajili wa marubani hao, unaolenga kurahisisha upatikanaji wa vibali na usajili wa ndege hizo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mfumo huo juzi jioni, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Daniel Malanga alisema kuanzishwa kwa mfumo huo kutafanya sasa upatikanaji wa vibali kutumia takribani wiki moja hadi mbili kutoka mwezi mmoja hadi miwili ya awali.

“Lengo la kujengwa kwa mfumo huu ni kuondoa kero waliyokuwa wakikutana nayo warushaji wa ndege hizo awali, hii ni kwa sababu upatikanaji wa vibali hivi ulikuwa ukihusisha taasisi nyingi.”

Awali mchakato huo ulikuwa ukifanyika kwa njia ya kawaida na ulimlazimu aliyehitaji kibali kupita katika ofisi mbalimbali kushughulikia suala lake, jambo lililochukua muda mrefu.

"Kwa biashara hii ni changamoto inayoathiri mwenendo wa biashara na leo utatatuliwa kwa mfumo mpya, hii ni baada ya TCAA kuamua kuwarahisishia watumiaji wa ndege hizi kwa kutekeleza mfumo utakaorahisisha mchakato wa upatikanaji vibali kuanzia usajili na matumizi," alisema.

Kusajiliwa kwao kunawapa uhalali wa wao kurusha ndege hizo katika maeneo tofauti nchini na kabla ya usajili mhusika atatakiwa kuhudhuria mafunzo maalumu kupitia chuo cha Civil Aviation Training Center kilicho chini ya TCAA.

Kwa mujibu wa utaratibu huu, waliosajiliwa ni wenye vyeti na wamefundishwa kuhusu kanuni, sheria na taratibu za usafiri wa anga, kwa kile kilichoelezwa kuwa drone siyo kamera, ni ndege na ni hatari kurushwa kiholela na watu wasiofahamu kanuni na taratibu.

Ibrahim Abraham, ambaye anajishughulisha na usimamizi wa ndege zisizo na rubani kutoka TCAA alisema wametoa vibali 300 kwa ajili ya kutumia drones na vibali 160 kwa ajili ya uingizaji.

“Lakini kuwepo kwa mfumo huu sasa mtu atakuwa akitaka kurusha drone yake ataingia tu huku na kutoa taarifa kuwa atafanya hivyo wapi na saa ngapi,” alisema Abraham.