Ushahidi kesi ya Sabaya: Shahidi aeleza alivyokimbilia kujificha Msikitini masaa matatu

Ushahidi kesi ya Sabaya: Shahidi aeleza alivyokimbilia kujificha Msikitini masaa matatu

Muktasari:

  • Kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya na wenzake wawili leo imeanza kusikilizwa huku shahidi wa kwanza alieleza alivyokimbia kujificha Msikitini.

Arusha. Kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya na wenzake wawili leo imeanza kusikilizwa huku shahidi wa kwanza alieleza alivyokimbia kujificha Msikitini.


Akitoa ushahidi katika kesi hiyo ya unyang'anyi wa kutumia silaha, shahidi ya kwanza, Mohamed Saad amesema alikimbilia Msikitini wa Kijenge baada ya Sabaya na wenzake kuingia dukani kwake na kumpa dakika tano afike dukani.


Shahidi huyo akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo alieleza Mahakama kuwa alikimbia kwa hofu kwani baada ya Sabaya kufika dukani kwake alipigiwa simu na ndugu yake Ally Saad kuwa Sabaya yupo dukani na amekuwa akiwasumbua wafanyabiashara.


Akiongozwa na wakili wa Serikali, Abdallah Chavula shahidi huyo amesema Februari 9, mwaka huu, Sabaya na wenzake walivamia dukani na kuchukua kiasi cha Sh 2,769,000 milioni.


Amesema baada ya Sabaya kuingia dukani na wenzake walijitambulisha kuwa ni maofisa wa Serikali ambapo walianza kumtafuta ndipo ndugu yake Noman Jasin alimpigia simu kuwa anatakiwa dukani.


Alisema wakati anazungumza naye ndipo Sabaya alichukuwa simu na kumtaka ndani ya dakika tano afike dukani.
Alisema alikimbia kwenda kujificha Msikiti wa Kijenge na alikaa kuanzia saa 12 jioni hadi saa mbili na baadaye alikwenda kulala kwa rafiki yake eneo la Esso Makaburini.


Alisema baada ya upekuzi wa Sabaya dukani na kuchukua fedha na mashine ya EFD walikwenda  hadi nyumbani kwake kufanya upekuzi.


Alisema alipigiwa simu na mke wake kuwa Sabaya na wenzake walivunja nyumba wakiwa na bastola na kuingia ndani wakimtafuta na wamesema hawatalala hadi  wampate.


Amesema kutokana na hofu alikimbilia Wilaya ya Simanjiro kujificha na baada alirudi Arusha Februari  17 mwaka huu na kuichukuwa familia yake na kuipeleka Nairobi nchini Kenya na inaishi huko hadi sasa.


Sehemu ya mahojiano na Wakili wa utetezi, Moses Mahuna ilikuwa hivi.


Mahuna: Kwanini ulipopigiwa simu uende dukani kwako hukwenda.
Shahidi: Nilisikia mabishano pale dukani ndio nikapata hofu.

Mahuna: Je? Baada ya tukio hilo uliliripoti polisi

Shahidi: Hapana.

Wakili Dancon Oola: Una uthibitisho gani kuwa Sabaya na wenzake waliiba Sh 2,769,000 milioni.

Shahidi: Niliwaona kwenye CCTV camera

Oola: Je wewe uliamini vipi kama wao ndio wameiba?

Shahidi: Niliambiwa na Noman Jasin.

Wakili: Je uliripoti polisi?

Shahidi: Sijaripoti lakini niliandika barua TRA

Wakili: Unasema Februari 17 ulirudi Arusha na kuipeleka familia Kenya, Je? Ulipima Covid maana siku hiyohiyo umetoka Simanjiro ulikwenda Nairobi.


Shahidi: Hapana.
Wakili Chavula aliieleza Mahakama kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha Sabaya na wenzake.