Utata wa vifo Rombo, Serikali yatoa tamko

Moshi. Ni ugonjwa gani uliowaua? Hili ndilo swali linaloumiza vichwa kwa sasa, baada ya Serikali kutoa tamko rasmi kuwa vifo vya watu watatu vilivyotokea siku 24 zilizopita wilayani Rombo, havikusababishwa na kula nyama yenye kimeta.

Bado kuna utata kuhusu idadi ya waliokufa na wale wanaodaiwa kuugua, kutokana na taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Jairy Khanga kueleza idadi ya waliokufa ni wawili na waliougua ni watu tisa tu.

Taarifa zilizotolewa awali zilidai watu watatu, wakiwemo wawili wa familia moja ambao ni mume na mke, walifariki dunia baada ya kula nyama msibani inayodhaniwa kuwa na kimeta katika kijiji cha Msaranga wilayani Rombo.

Tukio la kula chakula msibani lilitokea Mei 4, 2023 na hadi Mei 21, ilielezwa watu 188 waliokuwepo msibani hapo walipewa dawa kinga (Ciprofloxacin) kutokana na watu wengine 15 kudaiwa kuumwa tumbo, kuhara na kutapika.

Diwani wa kata hiyo, Mathias Assenga alikaririwa akisema tukio hilo lilikuwa limezua taharuki kubwa kutokana na baadhi ya watu kuendelea kuhara na wengine walioshiriki mazishi hayo waliendelea kuchunguzwa kwa ukaribu.

"Kulikuwa na mazishi mahali hapa kwenye kata yangu, ambayo yalifanyika kwa mzee mmoja aliyekuwa amefiwa na kijana wake, sasa wakati wa mazishi kuna mama alikuwepo anahudumia kule jikoni, ambaye pia alichukua na chakula na kupeleka nyumbani baada ya shughuli ya mazishi kumalizika," alidai.

"Chakula hicho baada ya kupeleka nyumbani alikula yeye na mume wake, mwali wake pamoja na mjukuu wake. Sasa siku iliyofuatia ambayo ni siku ya Ijumaa huyu mama alijisikia vibaya na siku ya Jumapili alipoenda hospitali alizidiwa na Jumatatu ya Mei 8 alifariki," alinukuliwa Diwani huyo akieleza.

"Lakini wakati huo tayari mume wake naye alikuwa ameshaanza kuharisha na alikuwa hospitalini na hakuweza kumzika mke wake, Alhamisi ya Mei 11 naye mume wake akafariki na mwali wake naye pia akawa amelazwa hospitalini.

"Sasa hii imeleta taharuki kidogo kwa sababu kuna kijana mwingine wa familia nyingine ambaye naye alikuwa anahudumia pale msibani naye akawa amekufa na alizikwa Mei 17 na wale wote ambao walikuwa wanaharisha walielekezwa kwenda hospitali," alieleza Assenga.

Kwa upande wake, Andrew Laswai ambaye ni muuguzi katika Hospitali ya Ngoyoni, alinukuliwa akisema Mei 16, 2023 hospitali hiyo ilipokea jumla ya wagonjwa 34 ambapo wanaume walikuwa 11 na wanawake 23.

“Tulipokea wanaume 11 na wanawake 23 ambao walipata dawa ya ‘Ciprofloxacin’ na walikwenda nyumbani na siku hiyo hiyo tukapokea wagonjwa wengine watatu, mwanamke mmoja na wanaume wawili ambao tuliwalaza wodini,” alisema.

Laswai alisema kuanzia siku ya kwanza hadi Mei 17, 2023 hospitali hiyo ilikuwa imepokea jumla ya wagonjwa 47 na kwamba katika uchunguzi na maelezo ya wagonjwa wenyewe ni kwamba walikula nyama ambayo ilihisiwa kuwa na kimeta.

Taarifa ya mganga mkuu mkoa

Akizungumza na gazeti hili juzi jioni, Dk Khanga alisema baada ya timu ya wataalamu kufanya uchunguzi, imebaini hakuna mlipuko wa kimeta wala kipindupindu katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.

"Timu ya wataalamu ya Mkoa ikishirikiana na timu ya watu wa mifugo, afya, maji na TBS (Shirika la Viwango Tanzania) tulifanya uchunguzi wa kina na kupeleka sampuli kwenye maabara za Taifa na matokeo yamekuja kwamba kile ambacho wananchi walikuwa wanakifikiri haikuwa kweli," alisema Dk Khanga.

"Wananchi walifikiri kuna ugonjwa wa kimeta, lakini majibu yanaonyesha hakuna kimeta wala hakuna kipindupindu, na wananchi waliougua walikuwa tisa na kati yao wawili walifariki na tunaamini ni matatizo ya mtu mmoja mmoja," alisisitiza.

"Kwa sababu hata ukiangalia walikula chakula Mei 4, mgonjwa wa kwanza alienda kulazwa Mei 7 na kufariki Mei 8 na mgonjwa wa pili alilazwa Mei 12, Kama kile chakula kingekuwa na matatizo, kisingeweza kuchukua kipindi hicho," alisema.

"Tunadhani ni matatizo ya mtu mmoja mmoja au ni matatizo ambayo yalitokana na uchafuzi uliotokana na source (chanzo) katika ngazi ya mtu mmoja mmoja lakini siyo katika common source (chanzo cha pamoja),” alieleza na kuongeza:

“Kwani tumejaribu kuangalia maji yako safi, vipimo tulivyofanya katika Hospitali ya rufaa ya Kanda KCMC na Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi viko safi, na hata vya maabara kuu ya Taifa viko safi.

“Kwa sasa Rombo hakuna tatizo na wagonjwa wote wameruhusiwa wako nyumbani na hakuna kisa kingine kilichoripotiwa. Naomba niwatoe hofu wananchi kwamba hali ni shwari na waendelee na shughuli zao za kawaida kwani hakuna mlipuko wa ugonjwa wowote Halmashauri ya Rombo," alisisitiza.

Alipoulizwa chanzo cha watu hao kupata ugonjwa wa kuhara, Dk Khanga alisema sababu za ugonjwa huo ziko nyingi, na haiwezekani kudai ni mlipuko unaoleta taharuki, huku akiongeza kuwa mtu anaweza kula chakula na kupata shida ya kuhara.

Nyongeza na Janet Joseph