Utekelezaji miradi ya CSR na mapambano dhidi ya rushwa

Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba akizungumza wakati wa warsha ya siku nne ya mapambano dhidi ya rushwa kwa makundi mbalimbali iliyoandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji madini ya Geita (GGML), kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (Takukuru) Mkoani Geita.

Muktasari:

  • Kupitia mafunzo hayo watumishi wa Serikali wataisimamia miradi yote inayonufaika na fedha za CSR kwa uwazi, lengo likiwa ni kukwepwa mianya na viashiria vya rushwa kwa manufaa ya wananchi.

Geita. Utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji wa Kampuni kwa jamii (CSR) mkoani Geita imetakiwa kwenda sambamba na mapambano dhidi ya rushwa kuanzia kwenye uibuaji wa mradi, namna ya kuwapata mafundi na makandarasi wenye ubora. Pia ununuzi wa vifaa ili kuwezesha miradi  hiyo kukamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Akizungumza kwenye warsha ya mapambano dhidi ya Rushwa iliyoandaliwa na Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML) kwa kushirikiana na Taasisi ya kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoani hapa, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba amesema Serikali imelenga kupambana na rushwa ili kupata miradi yenye tija inayoendana na thamani halisi ya fedha na itakayokamilika kwa wakati.

Amesema kampuni ya GGML imekuwa ikishirikiana na Serikali kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuwawezesha wazawa kupata zabuni ndani ya mgodi .

“Kwenye CSR kumekuwa na mashirikiano kati ya halmashauri na mgodi pamoja na wananchi wanaoibua miradi, lengo likiwa ni kuchochea maendeleo na ili miradi hii iweze kuwa na manufaa na tija jambo muhimu linalopaswa kutangulizwa ni mapambano dhidi ya rushwa.”

“Mapambano hayo yawe katika  uibuaji wa miradi, namna ya kuwapata mafundi na wakandarasi watakaozingatia uadilifu ikiwamo kumaliza  miradi kwa wakati na kwa ubora,” amesema.

Amesema,  “warsha hii itumike kutafakari namna ya kuongeza ufanisi kwenye miradi ya CSR, miongoni mwa vitu vitakavyofundishwa ni namna bora ya kuwa na mifumo ya manunuzi ambayo haitatawaliwa na rushwa na namna gani tunaweza kuwa na ukamilifu wa miradi ya CSR ili wananchi waone  matokeo kwa wakati,”amesema Komba.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat amesema ufisadi ni tishio kwa ukuaji wa uchumi duniani na inaathiri maendeleo ya nchi.


“Nina matumaini makubwa kwamba kufikia mwisho wa warsha hii, washiriki wote watakuwa wameongeza ufahamu juu ya hongo na ufisadi na kuwa na uelewa mzuri wa sera na viwango vya GGML vya kuzuia na kupambana na rushwa,” amesema Grat.

Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Azza Mtaita amesema kwa miaka mitatu sasa warsha hizo zimesaidia kuyafikia makundi mbalimbali ya watu, sambamba na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kukabiliana na rushwa hasa kwenye miradi CSR.

Lauton Changanya mmoja wa washiriki wa warsha hiyo amesema kupitia warsha hiyo watumishi wa Serikali watakuwa na uwezo wa kubaini na kuzuia mianya ya rushwa kwenye miradi ya SCR.