Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uundwaji Tume ya Jaji Lila  ulivyoibua mvutano mahakamani

Muktasari:

  • Tume hiyo imeundwa na Rais Samia, lakini wananchi wawili wameomba ruhusa ya Mahakama kupinga uteuzi wa makamishna wake



Dar es Salaam. Uundwaji wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, umeibua mvutano wa hoja za kisheria mahakamani baada ya Serikali kudai haiwezi kupingwa, kwa kuwa haijakamilika kuundwa.

Serikali imeibua hoja hiyo wakati wa usikilizwaji wa shauri la maombi ya ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya kimahakama kupinga uteuzi wa makamishna wa tume hiyo; leo Jumatatu, Juni 8, 2026 na Jaji Augustine Rwizile, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma.

Hata hivyo, mawakili wa wajibu maombi wameipinga hoja hiyo pamoja na kubainisha hawapingi tume bali uteuzi wa makamishna. Pia, wamehoji mawakili wa Serikali kama tume hiyo haijakamilika kuundwa kwa mujibu wa sheria iweje wameiwakilisha katika shauri hilo.

Tume hiyo maarufu Tume ya Jaji Lila, inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na makamishna wake walitangazwa Mei 18, 2026.

Makamishna hao wa tume hiyo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.

Rais Samia ameunda tume kufuatia ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Hata hivyo, mwanaharakati Buberwa Ephraim Buberwa na mwenzake Joseph Daud Mabugo, wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, wamefungua maombi kwa lengo la kupinga uamuzi huo.

Wamefungua shauri dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Lila na wajumbe wake watatu, Mjemmas, Bawazir na Sumari (mjibu maombi wa pili mpaka wa tano mtawalia).

Wanaomba ruhusa kufungua shauri la mapitio ya Mahakama (Judicial Review), kuiomba itengue uamuzi huo wa Rais Samia wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.

Shauri hilo limesikilizwa leo Jumatatu huku mawakili wa waombaji, Mpoki, akisaidiana na Mwasipu wameieleza Mahakama wateja wao wamekidhi vigezo vyote vitatu vya kupewa ruhusa hiyo kama vilivyokwisha kuwekwa na Mahakama.

Vigezo hivyo ni vya mwombaji kuonesha kuna hoja inayohitaji kujadiliwa na Mahakama, mwombaji kuonesha ana masilahi katika jambo au uamuzi unaolalamikiwa na mwisho maombi kufunguliwa ndani ya muda yaani miezi sita tangu kutolewa kwa uamuzi au kufanyika kwa jambo linalolalamikiwa.  

Majibu ya Serikali

Akijibu hoja hizo, ‎Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method kwa niaba ya jopo la mawakili Serikali waliowawakilisha wajibu maombi wote, AG na makamishna wa Tume hiyo amesema wanakubaliana na mawakili wa waombaji kuhusu masharti ya kupewa kibali hicho.

‎Hata hivyo, Vivian amedai waombaji hawajatimiza sharti moja wapo la kuthibitisha kuwepo kwa hoja inayohitaji kujadiliwa na Mahakama na kwamba kwa sababu hiyo inalifanya shauri hilo kutokuwa na ustahilifu wa kukubaliwa.

‎Amefafanua suala lililoko mahakamani ni kuhusu muundo wa tume kuchunguza ujinai katika matukio ya wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 na kwamba aya za kiapo cha waombaji ambazo mawakili wao wamezitaja, hazina maelezo ya kutosha kuonesha kuwepo hoja ya kujadiliwa.

‎"Tunasema hivyo kwa sababu masuala yanayolalamikiwa ya uundaji tume yanaongozwa na Sheria ya Tume za Uchunguzi," ameeleza Vivian.

‎Amesema kifungu cha 20 cha Sheria hiyo, kinaeleza ili tume ionekane imeundwa kisheria ni lazima iwe imetangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) ambako ndiko itafahamika kuwa imeundwa chini ya kifungu kipi, mawanda ya kazi na mamlaka ya hiyo tume.

‎"Tumepitia pleadings (nyaraka zote za shauri) kwa jumla wake za waombaji hatujaona sehemu ambako wameongelea gazeti ilikotangazwa hiyo tume wanayoilalamikia kuthibitisha kuwa kuna hoja ya kujadiliwa," amedai Vivian.

 ‎"Kutokuwepo taarifa hizo za gazeti hilo kwenye nyaraka zao ni rai yetu kwamba hizo taarifa ambazo wamezitoa zinabakia kuwa hisia tu." 

‎Huku akiirejesha Mahakama hiyo katika uamuzi wake kwenye shauri la Tenzi Anthon Nyundulwa dhidi Phillip Mpango, amesema Mahakama ilieleza hisia bila kujali ni kwa namna gani zinashawishi haziwezi kukidhi matakwa ya kuwepo hoja ya kujadiliwa.

‎Vivian amekiri wanatambua taarifa kwa umma iliyoambatanishwa na waombaji inayoelezea kuhusu kuundwa kwa tume wanayoilalamikia.

Hata hivyo, amesema hiyo ni taarifa tu ya uteuzi wa makamishna ambayo haiwezi kutumika kuhitimisha kwamba tume hiyo imeundwa kwa jukumu fulani chini ya kifungu fulani, kama sheria inavyotaka.

‎"Kwa hiyo tunachosema ni kwamba hili shauri limeletwa kabla ya wakati wake kwa kuzingatia hisia tu," amesema na kusisitiza katika mazingira hayo hata mambo wanayoyalalamikia ya ukiukwaji sheria, Mahakama haiwezi kuyaamua.

‎Wakili Vivian ameiomba Mahakama hiyo iongozwe na uamuzi wa mashauri mbalimbai ya Mahakama Kuu aliyoielekeza Mahakama ilikataa kutoa kibali kutokana na mwombaji kushindwa kuambatanisha nyaraka husika kuthibitisha kuwepo hoja ya kujadiliwa.

‎Wakili wa Serikali Mkuu, Stanley Kalokola, ameongeza kutokuwepo sheria inayoanzisha tume hizo kifungu cha 20 ndio kinasisitiza tume, kazi na mamlaka yake na kazi inayotakiwa kuifanya itatambulika itakapokuwa imetangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

"Hayo yakithibitishwa hapo, Mahakama inaweza kuwa na nguvu ya kupima hizo hoja zinazolalamikiwa kwamba aliyeiunda amevuka mipaka yake vinginevyo ni kama tulivyosema, Mahakama itakuwa inafanyia kazi hisia," amesema Kalokola.

Maelezo ya Mpoki

‎Akijibu hoja hizo, wakili Mpoki amesema katika shauri hilo wanaomba kutengua uteuzi wa makamishna walioteuliwa na Rais kinyume cha sheria.

‎Amesema taarifa ya kuwateua makamishna hao ipo na imetaja dhahiri kuwa wameteuliwa chini ya Sura ya 32.

‎Amefafanua kifungu kinachompa Rais mamlaka kuteua tume ni kimoja tu na kwamba taarifa ya uteuzi imetaja sura ya 32 ambayo ina kifungu kimoja tu kinachompa Rais mamlaka ya kuteua tume.

‎"Mheshimiwa Jaji, ukiangalia aya ya 12 ya kiapo cha pamoja wajibu maombi (makamishna wateule) wanakubali kuwa waliteuliwa na kuna taarifa kwa umma, ambacho ndicho tunakuja kukiomba hapa mahakamani ambacho wao wanakikubali." 

‎Kuhusu hoja kwamba madai hayo ni hisia tu, Wakili Mpoki ameeleza hata sheria, kanuni ya 4 ya Kanuni   GN 324/20214 inasema mtu mwenye masilahi au anaamini ameathirika na uamuzi anaweza kuomba mapitio ya Mahakama.

‎Amesisitiza wametaja sheria, ambayo ni sura ya 32, Katiba na kanuni ambazo zimekiukwa kwa kitendo tu cha uteuzi ambao wenyewe walioteuliwa wanaukubali na hivyo haoni ni vipi mtu anaweza kusema ni hisia, wakati sheria inaruhusu kuchukua hatua hata kabla ya tukio.

‎Kwa upande wake, Wakili Mwasipu amehoji kama mawakili wa Serikali wanasema kutokuwepo GN ni vigumu kujua tume imeundwa kwa sheria gani, ni vipi wanawawakilisha makamishna hao wakati uteuzi wao haujatangazwa katika Gazeti la Serikali.

‎"Katika aya ya 9 ya kiapo cha AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) wanakubali kuwa Rais amewateua hao makamishna na wateja wetu wanapinga uteuzi huo kama ilivyo ombi la kwanza kwenye hati ya madai, " amesema Mwasipu.

‎Amesema Mahakama itakapopitia aya zote za kiapo cha waombaji, zimeeleza mtitiriko wa mambo mpaka wamekuja hapa mahakamani.

"Kwa hiyo aya zote zina taarifa za kutosha kuonesha kuwepo hoja ya kujadiliwa," amesisitiza Mwasipu.

‎‎Jaji Rwizile baada ya kusikiliza hoja za pande zote amepanga kutoa uamuzi wake.


Endelea kufuatilia Mwananchi

Mwisho