Uvamizi wa tembo waibua wabunge 13

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Muktasari:

Uharibifu na mauaji yanayosababishwa na uvamizi wa tembo nchini katika makazi ya watu umewaibua wabunge 13 bungeni wakitaka Serikali ieleze ni hatua gani inachukua ili kuwanusuru watu na tatizo hilo.

Dodoma. Uharibifu na mauaji yanayosababishwa na uvamizi wa tembo nchini katika makazi ya watu umewaibua wabunge 13 bungeni wakitaka Serikali ieleze ni hatua gani inachukua ili kuwanusuru watu na tatizo hilo.

 Wabunge hao ambao walihoji maswali hayo bungeni leo Alhamisi Juni 30, 2022 ni pamoja na Hamis Taletale (Morogoro Kaskazini) Rashid Shangazi (Mlalo), Daniel Sillo (Babati Vijijini), Tunza Malapo (Viti Maalum), Leah Komanya (Meatu) na Daimu Mpakate (Tunduru Kusini).

Wengine ni Grace Tendega (Viti Maalum), Mwita Getere (Bunda), Ester Bulaya (Viti Maalum), Ritta Kabati (Viti Maalum), Ester Matiko (Viti Maalum, Yahaya Masare (Manyoni Magharibi) na Francis Ndulane (Kilwa Kaskazini).

Baadhi ya maswali hayo ambayo yalijibiwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ni lililoulizwa na Mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate ambaye amesema katika jimbo lake tembo wameweka kambi.

Amehoji Serikali ina mpango gani wa kuthibiti tembo wanaoendelea na kambi kwenye eneo hilo.

Akijibu swali hilo, Mary amesema watajenga kituo kimoja cha askari wanyamapori na kuwagiza watu wa maliasili katika mikoa ya nyanda za juu kuenda katika eneo hilo kuwatoa tembo na kuwarudisha kwenye eneo lao.

Naye Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahaya Masare amesema jimbo la Manyoni Magharibi linapakana na mapori ya akiba mawili na kwamba wanyama wamekuwa wakihamia katika vijiji jirani.

“Serikali inampango gani wa kuthibiti hawa tembo?”amehoji.

Akijibu swali hilo, Mary amesema wameshagundua shoroba na askari wameshaelekezwa kwenda kuwatoa wanyama hao ili warudi katika mapori hayo ambapo ndio halisi makazi halisi.

Mbunge wa Viti Maalum, Tunza Malapo amehoji Serikali inampango gani wa kuvuna tembo ili kupunguza vifo na madhara yanayotokana na tembo hao.

Mary akijibu swali hilo, amesema dhana ya watu wengi ni kwamba wanyama hao wameongezeka, jambo ambalo amesema sio kweli.

Amesema kabla ya kipindi hiki walikuwa wanateseka na ujangili ambapo mwaka 2009 kulikuwa na tembo 134,000, lakini hivi sasa kuna tembo 55,000 hadi 60,000.

“Wananchi wanasogea hifadhi na shughuli za binadamu na ndio maana kati ya Aprili na Julai ndio wanyama hawa wanavamia katika maeneo hayo wakati ambapo ni wa mavuno,”amesema.

Amesema tembo kwa kawaida wananusa harufu umbali wa kilometa 200 na kwamba wanyama hao huenda katika maeneo hayo kutokana na shoroba kuzibwa.

Tomotheo Mzava (Korogwe) amehoji ni lini Serikali itarekebisha viwango vya fidia kwa walioathiriwa na wanyama hao ili viendane na mazingira yaliyopo.

Naibu Waziri huyo amesema wamepokea malalamiko ya viwango hivyo kuwa havifanani na gharama za mazao.

“Mazao tunaingiza katika mchakato ili waweze kupitisha mabadiliko ya sheria hii ili tuweze kuongeza kiwango,”amehoji.

Mbunge wa Viti Maalum, Ester Matiko amehoji kwanini Serikali isilime mazao ikiwemo matikiti na mahindi katika hifadhi ili kuzuia wanyama kwenda katika makazi ya watu.

Akijibu swali hilo, Mary amesema kwa kulima mazao katika hifadhi, wataharibu mazingira na hata uoto wa asili kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amewashauri wakazi hao kuacha mita 500 kutoka katika hifadhi badala ya kujenga karibu na hifadhi.

Katika swali la msingi, Francis Ndulane (Kilwa Kaskazini) amehoji Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tembo wanaoharibu makazi na mashamba katika Kata za Kandawale na Miguruwe ambazo zinapatikana na Pori la Akiba Selous.

Akijibu swali hilo, Mary amesema wizara imeanza kujenga vituo vya askari wanyamapori katika maeneo mengi nchini kwa lengo la kuwa karibu na wananchi ili kuwadhibiti wanyama hao.

Aidha, amesema wizara imepata kibali cha kuajiri askari 600 ambao watasambazwa kwenye maeneo hatarishi.