UVCCM waonya wanaopanga safu kupitia chaguzi

Katibu wa UVCCM Taifa Kenan Kihongosi

Muktasari:

  • Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umeonya watendaji watakaopanga safu zao katika chaguzi za chama hicho ikiwemo nafasi ya mwenyekiti na makamu wake katika jumuiya hiyo.

Dodoma. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umeonya watendaji watakaopanga safu katika chaguzi za chama hicho ikiwemo nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Oktoba 3 mwaka huu, Katibu wa UVCCM Taifa Kenan Kihongosi amesema mtendaji yoyote atakaebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa sababu kanunu ipo zipo wazi.

“Niwaombe watendaji wenzangu ndani ya Wilaya wajikite katika kusimamia kanuni wasijikite katika kunadi wagombea kwani kufanya hivyo ni kinyume cha kanuni na ikibainika tutachukua hatua kali,” amesema.

Amesema usaili wa wagombea wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa jumuiya hiyo unatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 8 hadi 16 mwaka huu Jijini Dodoma.

Katika hatua nyingine, Kihongosi amesema jumla ya wanachama 556,381 ambao ni vijana wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama.

Amesema kwa ngazi ya Taifa pekee wanachama 1253 wameweza kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali ambapo wanaume ni 788 na wanawake 465

Amesema kuanzia Oktoba 8 mwaka huu   watafanya usaili katika nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti Taifa na Oktoba 9 mwaka huu utakuwa usaili wa wajumbe wa Baraza Kuu viti vitano.


Amesema Oktoba 11 mwaka huu utakuwa ni usaili kwa wagombea wa ujumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa viti vitano.

“Tunatoa wito kwa wagombea kuwahi mapema kama utaratibu ulivyo lazima waweze kuja na viambatanisho cheti cha kuzaliwa,kadi ya uanachama wa CCM na UVCCM, vyeti vya masomo.

“Sambamba na hilo kadi ya Nida ni muhimu kwa sababu lazima tuhakiki umri wa kila mgombea ambaye amechukua fomu kuwania nafasi kama huna kadi njoo na namba.

“Nitoe wito kwa ngazi ya Taifa kati ya vitu ambavyo tutakuja kuvisimamia ni pamoja na kadi ya Nida kwani mgonmbea hatakiwi kuzidi umri wa miaka 30,” amesema Katibu huyo.