UWT, Bawacha waungana maadhimisho miaka miwili ya Samia

Muktasari:

  • Leo Machi 19, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan amefikisha miaka miwili tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania. Ni baada ya aliyekuwa Rais John Magufuli kufariki dunia Machi 17, 2021, jijini Dar es Salaam. Sherehe za kumpongeza zinafanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam

Dar es Salaam. Ni mwendelezo wa maridhiano. Hivi ndivyo inaweza kuelezwa kwa kinachoendelea katika sherehe za maadhimisho ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Sherehe hizo zinafanyika leo Jumapili, Machi 19, 2023 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambazo zimeandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi  (UWT).

Pia, katika sherehe hizo wamehudhuria viongozi na wanachama wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) akiwemo Kaimu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Sharifa Suleiman, Devotha Minja na Spika wa Bunge la Wanawake wa Chadema, Susan Lyimo.

Viongozi hao wa Bawacha wamevalia sare zao za vitenge walionekana wamekaa viti vya mbele wakifuatilia kila kinachoendelea kwenye sherehe hizo za miaka miwili ya Rais Samia.

Hii ni mara ya kwanza kwa wanawake wa Chadema kushiriki kwenye shughuli ya wanawake wa CCM na hili limetokea kama mwendeleo wa dhana ya maridhiano ambayo ameiasisi Rais Samia, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.

Bawacha wameshiriki sherehe hizo ikiwa ni takribani wiki moja imepita tangu Rais Samia alipohudhuria sherehe za Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2023 zilizokuwa zimeandaliwa na Bawacha na kufanyikia Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika hotuba yake siku hiyo, Rais Samia alieleza kushiriki kwake kwenye kongamano hilo kunazidi kufungua milango ya ushirikiano na maridhiano yenye lengo la kuiunganisha nchi na kuendeleza mshikamano kwa wananchi wote.

“Nilipopata mwaliko wa kuja kwenye maadhimisho haya sikusita kwa sababu nikiwa Rais wa Tanzania kundi hili ni langu pia huwezi kuitwa na wananchi wako ukasem siji.

Nilifurahi kuja kwa sababu nilijua leo nitapata fursa ya kusikia Chadema wanasema nini na nimewasikia,” alisema Rais Samia huku akiwakaribisha nao kwenye sherehe hizi ambazo zinafanyika leo ikiwemo kuwapatia vitengo ambavyo vimevaliwa leo.

“Nimesikia hapa mnaaimba People’s power yani nguvu ya watu sasa nguvu hii ya wanawake wa Chadema ikaungane na kila chama cha siasa tukamkomboea mwanamke wa Tanzania, tukakuze uchumi. Twendeni tukaungane wote, tukianza kuweka mipaka hatutafika tukaunganishe nguvu tukatatue changamoto zilizopo.”