Vibanda 148 vyateketea kwa moto, Soko la Mitumba Kigoma

Muktasari:

Zaidi ya vibanda 148 vya soko la mitumba Manispaa ya Kigoma Ujiji, vimeteketea usiku wa kuamkia leo baada ya moto unaodhaniwa kusababishwa na hitilafu ya umeme kuzuka ghafla. 

Kigoma. Vibanda 148 vya Soko la Mitumba lililopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, vimeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo, huku chanzo cha moto kikidaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.

Akizungumza leo Februari 10, 2024 Kamanda wa Jeshi la Zimamoto mkoani  Kigoma, Jacob Chacha amesema saa nane kasoro usiku walipokea taarifa ya moto katika soko hilo la wafanyabiashara wadogo wa mitumba.

Amesema jeshi hilo lilifika eneo la tukio  baada ya kupata taarifa hizo na kukuta moto umesambaa eneo kubwa na walianza kukabiliana nao, ili usisambae na kuleta athari zaidi.

Kwa mujibu wa kamanda huyo taarifa ya awali inaonyesha kuwa ni hitilafu ya umeme ambapo tayari jeshi hilo limeanza uchunguzi wa kina wa tukio hilo.

 “Baada ya kuona moto huo umekuwa mkubwa tuliongeza magari kwa ajili ya kuendelea kuzima, tulifanikiwa kuudhibiti moto na hakuna madhara kwa binadamu,” amesema Chacha.

Amesema vibanda hivyo vinaanzia block A hadi J  na  sehemu iliyoathirika zaidi ni eneo la block J ambayo ina jumla ya vibanda 148, kati ya hivyo 111 vilikuwa na bidhaa na  vingine 37 vilikuwa bado havijaanza kufanyiwa  biashara.

Chacha amesema kuanzia block A hadi J ilikuwa na jumla ya vibanda 727, vibanda 377 vilikuwa na biashara na vilivyosalia  vilikuwa havina bidhaa wala biashara ya aina yoyote.

Baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo, wameiomba Serikali kufuatilia suala la uunganishwaji wa umeme katika vibanda hivyo.

Rashid Mtawala amesema bado haijathibitishwa kuwa chanzo cha moto nini lakini kumekuwa na tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kujiunganishia umeme wenyewe kwenye vibanda, bila kutoa taarifa kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

“Sijasema kuwa  umeme ndio chanzo cha moto hapana, tunasubiri mamlaka iweze kutoa taarifa rasmi lakini kujiunganishia umeme bila kufuata utaratibu kunaweza kusababisha hali ya vibanda kuwaka moto kama ilivyotokea leo,”amesema Mtawala.

Rashid Bungona amesema hadi sasa hajui cha kufanya kutokana na mali zake zote iangalie  namna ya kuwasaidia, kwani wengi wao wamechukua mikopo.