VIDEO: Alichokisema Rais Magufuli ibada ya mwisho kuhudhuria St Peter Dar

Alichokisema Rais Magufuli ibadani St Peter Dar

Muktasari:

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

“Tumsifu Yesu Kristo, Tumsifu Yesu Kristo” Rais wa Tanzania, John Magufuli alianza kusema hivyo alipohudhuria mara ya mwisho misa katika kanisa la St Peter jijini Dar es Salaam.

Akiwa katika ibada hiyo aliendelea kusema, “Napenda kuwatakiwa heri ya mwaka mpya wanaparokia wote wa mtakatifu Petro kwa sababu tangu mwaka jana sijawahi kuja hapa, nimekuwa vijijini kule, basi nawatakia heri ya mwaka mpya,” salamu hizo za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilipokelewa kwa makofi na waumini waliokuwa wamehudhuria ibada hiyo.

Rais John Magufuli aliendelea kwa kumpa pole paroko wa kanisa hilo kwa kuondokewa na mama yake kipenzi ambaye alifariki wiki mbili zilizopita na kumtakia Mungu ampumzishe kwa amani.

“Kwa hiyo natoa pole kwako na wote wanamuhusu marehemu mama Makubi.”

“Ndugu wangu wakristo tuko katika kipindi cha Kwaresma, kama alivyozungumza baba paroko hii ni wiki ya kwanza ya kwaresma na kwaresma ina historia kubwa hata ya majaribu ya shetani ambaye alimjaribu hata bwana wetu Yesu Kristo.”

“Kama bwana Yesu alijaribiwa kwa siku arobaini mimi na wewe tu nani mbele ya shetani? Alihoji Rais Magufuli akiendela kutoa hotuba katika misa hiyo iliyofanyika Februari 21 mwaka huu.

Nizidi kuwapa moyo wenzangu wakristo pamoja na wa madhehebu mengine na Watanzania kwa ujumla kwamba kimbilio letu ni Mungu.

“Nimeshukuru sana waimbaji hapa walipokuwa wakiimba hawakuangaika hata kuvaa barakoa kwa kuwa wanajua Mungu wao ni mkubwa kuliko barakoa.”

Sijasema wanaovaa barakoa wanafanya vibaya,” aliendelea kusema Rais John Magufuli huku akipigiwa makofi na waumini huku naye akicheka na kusema, “hata wewe baba paroko, umekuja bila kuvaa barakoa, ilipofika wakati mwafaka wa kuvaa barakoa ulivaa na hatimaye sasa umeivua, hii inaleta Imani kubwa sana.”

“Ndugu zangu, nchi nyingi zimeanza kuvaa barakoa na ninyi wenyewe ni mashahidi kwenye vyombo vya habari, nchi hizo ndizo zinazoongoza kwa watu wengi kufa, wengi maelfu. Sijasema msivae barakoa, wala msinikoti vibaya lakini kuna barakoa nyingine siyo nzuri.”

Aliendela kuzungumza Rais John Magufuli kwamba, “Nataka niwaambie huu ndiyo ukweli, mtaletewa barakoa nyingine ndizo zenye matatizo, mimi ni kiongozi wenu ninajua mengi ni lazima niwaambie ukweli.”

“Ukitaka kuvaa barakoa kavae zilizotengenezwa na wizara ya afya, MSD wanatengeneza barakoa, ukishindwa za namna hiyo shona yako mwenyewe, kachukue likitambaa hata kama ni kanga likunje hata mara tano, mimi ni mwenzenu ninaifahamu hii ni vita na ndiyo maana mtaona wagonjwa wengi ambao wameathirika na magonjwa haya ya corona wako mjini.”

“Vijijini kule kwa mheshimiwa Jaji Mihayo hawapo wanaovaa barakoa ndiyo maana hawaathiriki, nilikuwa namuangalia Jaji Mihayo hapa amefunika pua yake na mke wake mpaka nilishindwa kuwaelewa mwanzoni, lakini maandiko yanasema kila atakayetaka kuiokoa nafsi yake ataipoteza,” aliendelea kusema Rais wa Tanzania, John Magufuli huku waumini wakimsikiliza kwa makini.

“Ninawaomba sana ndugu zangu Watanzania ndugu zangu wakristo tujue Mungu yupo, tujue Mungu yupo, tusiogope tujue iko siku tutakufa, hata mimi nitakufa tujue alichokipanga Mungu, naweza nikafa kwa corona naweza nikafa kwa nini ndiyo maana hata mimi sijavaa barakoa, siyo kwamba siogopi kufa, nimeona niliseme hili,”

Namshukuru hata sista hapa hajavaa lakini wenzake wawili wamevaa nikasema sasa kama hawa viongozi kila siku wanasema tumwamini Mungu vipi leo? Alihoji Rais John Magufuli na kuendelea, “Mungu anaweza.”

“Tutaokolewa kwa neema, ninawaomba Serikali haijazuia barakoa lakini tuwe waangalifu barakoa ipi tunavaa, tutaangamia, msifikiri tunapendwa mno, vita ya uchumi ni mbaya, ndiyo maana ninawapongeza watu waliovaa barakoa za kutengeneza wao.”

“Hizi wanazonunua madukani, tunajimaliza wenyewe, lazima niliseme najua watatukana sana lakini nina wajibu wa kusema ukweli, hebu tutaje ni nchi gani ambayo hawajafa watu na corona, maelfu wanakufa, kuna nchi iliwahi kupoteza watu 3000 kwa siku moja na wanavaa barakoa mbilimbili, sisi tuchukue tahadhari za kiafya kama zinavyotangazwa, tumtangulize Mungu lakini tutafute mbadala kama kujifukizia, wako mimi hata wasaidizi wangu wameshaugua, mimi watoto wangu wameshaugua, wapo wadogo zangu wameshaugua ni kumtanguliza Mungu.”