VIDEO: Askofu Shoo amaliza mgogoro Dayosisi ya Kusini Mashariki
Muktasari:
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fredrick Shoo amefanya ziara ya siku tatu mkoani Mtwara kwa ajili ya kutatua mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka sita.
Mtwara. Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fredrick Shoo amefanya ziara ya siku tatu mkoani Mtwara kwa ajili ya kutatua mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka sita.
Akizungumza jana Jumatano Machi Mosi, 2023 baada ya kumaliza kwa vikao vinne vilivyofanyika kwa siku mbili Askofu Shoo amekiri kuwepo kwa migogoro katika Dayosisi mbalimbali Tanzania.
Amesema kuwa wameunda kamati ya watu 11 kwaajili ya kuandaa mkutano mkuu utakaosimamia uchaguzi wa Askofu mpya pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya Dayosisi ya Kusini Mashariki.
“Huu mgogoro ni kweli umechukua muda mrefu lakini sisi kama viongozi hatujakaa kimya mara kadhaa tulituma viongozi wa kanisa zaidi ya mara mbili ambao waliofika na kuwaelekeza lakini mgogoro haukuisha sisi tunaamini hatukukaa kimya ila tulishauriana na kumuomba Mungu atupe njia sahihi ya kuutatua mgogoro huu,” amesema Askofu Shoo.
Naye Askofu wa Dayosisi ya Kusini Mashariki wa KKKT, Lucas Mbedule Judah amesema kuwa ameridhia kustaafu ambapo ataendelea kuwa askofu mpaka mkutano mkuu wa Julai utakaomchagua mrithi wa kiti chake.
“Migogoro ipo hata kwenye ndoa, lakini nimekuwa jasiri kwa muda mrefu. Nimepambana na uongozi, lakini hatima yake nimeona nipumzike kwa kuomba kustaafu, kikubwa nawaombea wanapopata askofu mpya wasiwe na migogoro yoyote na wasije kuachia njiani,” amesema Askofu Mbedule