VIDEO: Chadema kupiga marufuku kutumika jina na nembo yao Uchaguzi Serikali za Mitaa

Naibu Katibu mkuu Bara John Mnyika akionyesha form za uchaguzi akizungumza na wandishi wa habari kuhusu kujitoa kwa chama hicho  katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchi nzima Picha na Omar Fungo


Muktasari:

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Bara, John Mnyika amesema chama hicho kitamwandikia barua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupiga marufuku kutumika kwa jina na nembo ya chama hicho kwenye mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kesho kinamwandikia barua Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo kuacha kutumia jina na nembo ya Chadema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu chama hicho kimejitoa.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumapili Novemba 10, 2019 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Bara, John Mnyika amesema chama hicho kimejitoa kwa sababu ya dhuluma zilizofanyika kwenye mchakato mzima.

“Sisi kama chama tutamwandikia barua Waziri Jafo ya kumpiga marufuku kulitumia jina la Chadema au nembo yake katika mchakato wa uchaguzi kwa sababu tumejitoa,” amesema Mnyika.

Pia, amewataka wagombea waliopitishwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kuendelea kuwasilisha barua za kujitoa kwa sababu ndiyo msimamo wa Kamati Kuu ya chama hicho.

Amesema Kanuni ya 14 na 15 ya uchaguzi huo, inaelekeza mgombea wa uchaguzi lazima adhaminiwe na chama cha siasa, hivyo, kauli ya Jafo kuwatambua wagombea waliopitishwa ni upotoshaji.

Ametoa wito kwa wanachama wa Chadema na Watanzania kwa ujumla kupuuzia wito wa Waziri huyo na kutekeleza uamuzi wa Kamati Kuu ya chama yaliyofanyika Novemba 7, mwaka huu.