VIDEO: Hali ilivyo nyumbani kwa Lowassa, ujenzi wa kaburi wakamilika
Muktasari:
- Viongozi wa kisiasa, kimila na wananchi wapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Lowassa, ujenzi wa kaburi atakalozikwa wakamilka.
Monduli. Mamia ya watu wanaendelea kujitokeza nyumbani kwa Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa (70) nyumbani kwake Kijiji cha Ngarash, wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.
Shughuli zinazofanyika hapa nyumbani kwake leo Ijumaa, Februari 16, 2024 ni ibada fupi iliyoanza asubuhi inayoenda sanjari na salamu kutoka kwa viongozi wa kisiasa na kimila.
Pia, wananchi wa Monduli na viunga vyake watauaga mwili wa kiongozi huyo kuanzia leo asubuhi hadi 12 jioni. Kabla ya hapo, utaagwa na kimila na Malaigwan.
Watu wengi wamejitokeza nyumbani hapo, wakiwemo viongozi wakiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama.
Saa 9.25 asubuhi, mwili wa Lowassa ulitolewa ndani ya nyumba na kuwekwa kwenye hema maalumu litalotumika kwa ajili ya kumuaga.
Kabla ya kuanza kuagwa, kumefanyika ibada iliyoongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel.
Salamu kutoka kwa viongozi wa dini, kimila, vyama vya siasa, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na viongozi zimetolewa kwa kila kundi kumwelezea jinsi walivyomfahamu Lowassa enzi za uhai wake.
Asimilia kubwa ya waombolezaji waliowasili nyumbani hapo ni kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Mabasi kadhaa ya 'Friends of Lowassa', yameonekana nje katika eneo la kuegesha magari, huku wenyeji wa eneo hilo nao wakiwasili nyumbani hapo.
Mwili wa mwanasiasa huyo ulianza kuagwa kitaifa Februari 13, 2024 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na siku iliyofuata ilikuwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Azania Front alipokuwa akisali enzi za uhai wake akiwapo Dar es Salaam.
Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2024 akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alipokuwa akipatiwa matibabu ya magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.
Mhagama, Pinda
Waziri Mhagama amesema ndani ya Serikali kuna mambo Lowassa ameacha kama alama akiwa mtumishi na mtendaji ndani ya Serikali.
"Kwa niaba ya Serikali tunaipa pole familia, Lowassa alikuwa mtu wa watu, ana marafiki wengi. Matunda na alama aliyoiacha inatugusa kwa umoja wa kitaifa, sisi kama Serikali na tutaendelea kutambua yote aliyoacha akiwa mtumishi na mtendaji ndani ya Serikali, tunaungana na kujifunza kutoka na mifano mema aliyofanya katika uhai wake," amesema.
Waziri Mkuu mstaafu, Pinda amesema yako mengi Lowassa aliyofanya enzi za uhai wake na Watanzania wanapaswa kuyaenzi na kuona namna ya kuyasimamia.
"Binafsi nina nafasi ya pekee kwake, kwani alipokuwa Waziri Mkuu nikiwa chini yake nilijifunza mengi, alikuwa kiongozi anayejua kusimamia kile anachokiamini na kinafanyika, tumeondokewa na mtu ambaye tulijua mchango wake," amesema.
"Hatua aliyofikia Lowassa inahitaji maombi kuliko kitu kingine chochote. Kwa ibada hii ametukumbusha sisi wengine kwamba pamoja na mengine tutakayosema kuhusu Lowassa, ila alipofika iwe ni wajibu wetu na kama tunataka kuonyesha upendo kwake kila unapopata nafasi tumkumbuke na kumuombea," amesema.
Ajengewe mnara
Mkazi wa Ngarash, Fadhili Saidi amesema Lowassa amefanya mambo mengi kwenye elimu, afya na miradi mingine ya maendeleo kijijini hapo, hivyo anashauri ajengewe mnara hata kwenye ofisi ya CCM.
Saidi amesema enzi za uhai wake, Lowassa amewasaidia wananchi wengi kijijini hapo kwenda shule, akiwemo yeye kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne.
"Yaani bila yeye mimi nisingeenda shule. Nimesoma kwa msaada wake, amewasomesha wengi hapa kijijini. Amefanya mengi kwenye afya na miradi mingine ya maendeleo. Sasa kwa nini tusimjengee hata mnara hapa wa kumkumbuka?" amehoji.
Naye Famka Rabin, Mkazi wa Mvomero mkoani Morogoro ambaye ni jamii ya Kimasai amesema: "Tumempoteza mzee wetu. Alisisitiza sana sisi Wamasai kuhusu elimu, tufuge mifugo lakini tuhakikishe tunakwenda shule."
Naye Thomas Kahando amesema: "Tumeumia sana. Tumempoteza baba yetu. Kwa kweli umeumiama sana."
Eneo atakalozikwa, TV kubwa zafungwa
Kwa asilimia kubwa, maandalizi ya kaburi yamekamilika. Ujenzi umefanywa na Jeshi.
Kaburi lenye rangi nyeusi, unaweza kulifananisha na makaburi waliyozikwa marais wastaafu wa Tanzania, Dk John Magufuli na Benjamin Mkapa.
Kinachofanyika sasa ni maandalizi ya hema na mpangilio mwingine wa kiprotokali, kwani maziko yatahusisha viongozi akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.
Kutokana na wingi wa watu pamoja na mpangilio ulivyo, televisheni kubwa zimefungwa maeneo mbalimbali nyumbani hapo, ili kuhakikisha kila aliyefika anashuhudia.
Mahema mengine na televisheni zimefungwa kwa nje kabisa ambako waombolezaji wamekaa.
Pia, huduma ya intaneti katika eneo hilo inapatikana bure baada ya kufungwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali.