VIDEO: Korti yaamuru nyumba iuzwe kulipa mahari

Meatu. Mahakama ya Wilaya ya Meatu imeamuru nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Nkoma Mkoa wa Simiyu, Seleman Mussa (65), kuuzwa ili kulipa deni la Sh1.1 milioni analodaiwa kukamilisha mahari ya kijana wake.

Akizungumza na gazeti hili juzi baada ya hukumu kutolewa Machi 14 mwaka huu, Mussa alisema kijana wake ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari mkoani Shinyanga alimuoa binti wa Mwita Kati (Justina), wana mtoto mmoja na maelewano mazuri.

Kijana huyo alimuoa Justina mwaka 2019 na ndoa ya kimila kwa makubaliano ya mahari ya ng’ombe 15. “Tulikubaliana mahari ya ng’ombe 15 kwa thamani ya Sh150,000 kila mmoja, baada ya maridhiano walikuja nyumbani wakasema wanataka mahari yote, lakini tuliwaomba wachukue nusu (Sh1.1 milioni) na inayobaki tutailipa baadaye,” alisema Mussa.

Akisimulia alisema ilipofika mwaka 2020, baba mzazi wa mwanamke huyo alianza kudai mahari iliyosalia, ndipo alipoomba muda wa kuendelea kutafuta pesa kwa kuwa hakuwa na pesa wakati huo na ndipo ugomvi ulipoanzia.

“Hakuelewa, alitaka nimlipe pesa yote iliyobaki Sh1,125,000, tukaanza kutafuta muafaka katika vikao vya familia nikiomba kuongezewa muda ili niweze kutafuta pesa ya kumlipa,” alisema Mussa.

Pia, alisema walianza na vikao vya familia, viliposhindwa kupata muafaka walihamia katika ngazi ya Serikali ya kijiji hadi wakafikia hatua ya kupelekana mahakamani huku yeye (mtuhumiwa) akikimbilia katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Meatu kutafuta suluhu.

“Novemba 10, 2022 tulifika kwa Mkuu wa Wilaya Meatu, Fauzia Hamidu, huko niliahidi kupunguza na akatushauri turudi kwenye familia tukayamalize, nilipopata pesa nilienda kupunguza deni mbele ya Serikali ya kijiji kama mashahidi.”

VIDEO: Korti yaamuru nyumba iuzwe kulipa mahari

Mtifuano mahakamani

Shauri la madai lilifunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo, Meatu na kupewa namba 81 ya mwaka 2020 na ilitolewa hukumu katika Mahakama iliyoketi chini ya Hakimu F. F. Madungu Mach 14, 2023.

Katika hati ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Meatu ilieleza hukumu ya Mahakama ya Mwanzo ilikuwa kukamata nyumba ya Mussa namba 27B iliyopo Kijiji cha Nkoma ili kufidia Sh1.1 milioni kufikia Sh2.2milioni walizokubaliana.

Katika hati hiyo Mahakama ya Wilaya ya Meatu imeeleza kuwa mdaiwa aliomba kuilipa pesa hiyo kidogo kidogo hadi Septemba, 2023 na mdai alikataa na kutaka pesa yake kwa pamoja.

Mdai aliiandikia barua mahakama akiomba kukamata nyumba ya mdaiwa kwa kuwa hajalipa Sh1.1 milioni za mahari na mdaiwa alipelekewa samasi ya wito ikimtaka kufika mahakamani Julai 7, 2022 aeleze kwa nini ombi la mdai lisikubaliwe kama hataki kulipa.

Baada ya mdaiwa kusomewa barua ya maombi ya mdai, alisema deni litalipwa na mkwe wa mdai na mdai aliomba aendelee na utekelezaji wa ombi kwa kuwa mdaiwa hataki kulipa.

Mahakama ilikubaliana na ombi la mdai na ilitoa amri ya utekelezaji chini ya kanuni 56, GN: 310/1964, RE,2019, na hati za utekelezaji zipelekwe kwa ofisa mtendaji wa Kata ya Nkoma, Boniphace William ili zoezi liendelee.

William alisema awali alipokea hati ya kumtaka kuandaa hati za utekelezaji wa amri ya Mahakama, lakini mdaiwa amekuwa akisumbua.

“Hataki nyumba yake iuzwe, amekuwa akienda kwa viongozi mbalimbali wa chama na Serikali kutafuta suluhu lakini ni vyema akatekeleza agizo la Mahakama,” alisema Boniphace.


Anayedai afunguka

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Mwita Kati alisema anataka pesa yake ilipwe kwa kuwa ni miaka mitatu sasa amekuwa akidai pesa hiyo bila mafanikio.

“Tulikwenda Mahakama ya Mwanzo nikamshinda, Mahakama ya Wilaya nimemshinda sasa nipo sifahamu pesa yangu nitalipwa lini na tunasubiri siku 30 za kukata rufaa ziishe nianze kufuata hatua nyingine,” alisema Mwita Kati.

Samwel Christian, dalali wa Mahakama Mkoa wa Simiyu akizungumza kwa simu alisema bado hajapokea oda ya Mahakama kuhusu utekelezaji wa amri hiyo.