VIDEO: Mama asimulia maisha ya mtoto wake asiye na fuvu

Dar es Salaam. Msemo wa “Hujafa hujaumbika,” unasadifu hali ya Hussein Shaban, ambaye mwaka takribani wa tatu sasa, anaishi bila fuvu la mbele baada ya kupata ajali ya pikipiki Julai 19, 2020.

Hali hiyo imemfanya kuwa tegemezi kwa asilimia 100, kwa kuwa hawezi kuongea, kutembea, kula mwenyewe na hata kuhisi haja.

Mama mzazi, Dotto Salum ndiye mwangalizi pekee wa mtoto wake huku muda mrefu anautumia kumhudumia na kusababisha kuyumba kiuchumi katika familia.

“Naomba Watanzania wanisaidie, nina hali ngumu, sipati muda wa kufanya kazi zangu ili kuweza kumudu gharama za kumhudumia mgonjwa, ikiwamo kumpeleka kliniki ya mazoezi ya viungo kila wiki inayohitaji Sh100,000 na dawa za degedege,” anasema mzazi huyo alivyoanza kusimulia hali ya Hussein (29).

Mama huyo anayeamini kila kitu kitakuwa sawa siku moja na akiwa na huzuni usoni mwake, anasema, usiku wa Julai 19, 2020 hatakuja kuusahau katika maisha yake.

Siku hiyo ilibadili kila kitu ndani ya familia yake na ilimfanya kijana wake, Hussein aliyekuwa ameshaanza kujitegemea kurudi nyumbani na kuhitaji uangalizi sawa na ule wa mtoto mdogo asiyeweza kuzungumza.

Akiwa katika kazi yake ya udereva wa bodaboda usiku huo bila kujua kitu gani kitatokea mbele, abiria wawili aliokuwa amewabeba walimuomba asimame ili wanunue bidhaa katika moja ya maduka yaliyopo Kivule jijini Dar es Salaam.

Dotto anasema wakati mwanaye amesimama waligongwa na bodaboda nyingine iliyotokea mbele yao.

Akiwa amelala bila kujua kinachoendelea nje, alifuatwa na watu ili akamuone mwanaye, juhudi za haraka zilifanyika, ikiwamo kumchukua Hussein kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Amana na baada ya uchunguzi alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Tulipofika walimchunguza usiku ule na kuona kweli ameumia, walimfanyia upasuaji usiku huohuo, sikujua ni upasuaji upi, asubuhi nilimuangalia hali yake ikiwa mbaya Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), alipokaa baada ya wiki moja na nusu ndipo niliitwa,” anasema mzazi huyo.

“Nilipoitwa niliambiwa unajua mwanao ameumia sana, nikawaambia ndiyo, wakaniambia kuumia huko tumetoa fuvu lake la kichwa la mbele, ubongo ulikuwa unataka kuvimba, hivyo kumnusuru walilazimika kumtoa ili upate hewa.”

Mama asimulia maisha ya mtoto wake asiye na fuvu

Anasema hali hiyo ilimfanya kuhoji ni vipi mwanaye ataishi, huku wakimtoa hofu kuwa pindi atakapokaa sawa anatawekewa cement katika eneo ambalo fuvu limetolewa ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.

“Nilihoji kuhusu kumbukumbu zake waliniambia zitarudi ndani ya kipindi fulani kwa sababu ameumia sana,” anasimulia Dotto.

Anasema alimuuguza mwanaye hadi alipopata ahueni na kuruhusiwa kurudi nyumbani na tangu hapo hakuwahi kusikia neno lolote tena kutoka kwa mwanaye.

“Hawezi kula namlisha, namsaidia kila kitu, hadi sasa nakumbwa na changamoto nyingi kwa sababu mimi ndiyo mtafutaji, baba yake nilitengana naye tangu Hussein akiwa na mwaka mmoja, nimemlea mwenyewe hadi sasa.”

Dotto anasema moja ya changamoto anazokutana nazo ni namna ya kumhudumia mwanaye hasa katika upande wa ‘pampers’ kwa ajili ya kumsitiri, huku akieleza kuwa kukosekana kwake kumesababisha amalize vitenge vyake.

“Pampers zikiisha nimekuwa nikichana vitenge vyangu ili nimsitiri, hapo alipo nimechana naironi nimemfunga ili kuweka unadhifu, sina chochote kwa ajili ya kumhudumia huyu mtoto,” anasema Dotto.


Gharama ya kliniki

Mama huyo anasema amekuwa akikosa hela kwa ajili ya kumpeleka katika kliniki ya mazoezi Muhimbili ili afanyiwe mazoezi ya mguu na mkono ulioumia sana katika ajali.

“Natakiwa kwenda kliniki kila wiki, nikisema niende natakiwa niwe na Sh100,000, kati ya hiyo Sh60,000 ni kwa ajili ya kukodi gari ya kutupeleka kutusubiri na kuturudisha, Sh30,000 ni kwa ajili ya mazoezi na Sh10,000 ni kwa ajili ya akiba,” anasema.

Gharama hizo zinatokana na bima ndogo aliyonayo mwanaye inayoshindwa kugharamia huduma za mazoezi hayo, jambo ambalo limekuwa likisababisha akose kliniki kila wakati.

“Natakiwa kwenda kila wiki, ugumu wa maisha ilibidi niombe kwenda mara moja kwa mwezi, hata hiyo mara moja kwa mwezi nayo imekuwa ngumu, imefika kipindi nimeomba niende mara moja ndani ya miezi miwili hadi mitatu,” anasema.

Pia, anasema licha ya kumhudumia mwanaye kuathiri shughuli za kibiashara, kuna wakati inapaswa atoke kwenda katika shughuli zake za kukaanga samaki ili kupata kiasi kidogo cha pesa.

“Kuna wakati dada yake amekuwa akisaidia kwenda katika biashara zangu japo si mara nyingi kwa sababu mtaji umekuwa ukiathiriwa na matibabu.”

Dotto anasema ajali hiyo imesababisha mwanaye kuathiriwa na ugonjwa wa degedege, jambo ambalo limeongeza gharama nyingine za ununuzi wa dawa.

“Sasa hivi ufahamu unarudi kidogo, anaweza kujisogeza mwenyewe, ukimuita ukimuambia kitu anasikia na kutekeleza, japokuwa kuna vitu vikitendeka anakuwa hajui afanye nini,” anasema Dotto.


Matumaini ya bibi

Mbali na mama mzazi, Halima Kondo, bibi wa kijana huyo pia ana imani mjukuu atainuka na kurejea katika hali ya kawaida.

“Nimemlea mimi huyu mtoto tangu akiwa mdogo, hili lililotokea ni changamoto ya maisha ninayoamini itapita, hakuwahi kuwa na tabia mbaya yenye kukera, kijana mtiifu aliyejituma na upendo wa hali ya juu kwangu na ndugu zake,” anasema Halima.

“Hussein ni uzao wa tatu katika tumbo la mama yake akiwa na pacha mwenzie Hassan, ambaye pia ana maisha yake wakiwa nyuma ya ndugu zao wengine pacha ambao wametanguliwa na dada yao mkubwa.


Kama umeguswa kumchagia Hussein unaweza kuwasiliana na mama yake kwa namba 0782505208 jina litatoka Halima Kondo.