VIDEO: Mama atoa ya moyoni kupoteza wanaye wanne ajalini

Liliani Msuya (Katikati aliyejitanda mtandio mweupe)ambaye ni mama mzazi wa watoto wanne waliofariki katika ajali ya gari, mkoani pwani,  akilia kwa uchungu nyumbani nyumbani kwake Kijiji cha Kisangeni, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Watu hao wanne wa familia moja, walifariki Agosti 2, 2023 kwa ajali ya gari katika eneo la Mbewe, wakati wakitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Mwanga, kwenye msiba wa mdogo wao.

Mwanga. Wazazi wa watoto wanne waliofariki kwa ajali ya gari, Mbwewe mkoani Pwani, wameelezea namna walivyopokea taarifa za vifo vya watoto wao na kusema kuwa ni pigo ambalo halitasahaulika katika maisha yao.

Watu hao wanne wa familia moja, walifariki jana Aogosti 3, 2023 kwa ajali ya gari katika eneo la Mbewe, wakati wakitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Mwanga, kwenye msiba wa mdogo wao, ambaye ni mtoto wa baba yao mdogo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, leo Ijumaa Agosti 4, 2023, baba na mama wa watoto hao, wamesema waliishi na watoto wao kwa upendo na walikuwa tegemeo lao hasa katika kipindi hiki ambacho wamezeeka.

Liliani Msuya ambaye ni mama wa watoto hao, amesema ni pigo kubwa kuwapoteza watoto wake wote na kwamba hana cha kufanya ila anamuachia Mungu.

Rose Mwange ambaye ni dada mkubwa wa familia akiwa ni mtoto wa baba mkubwa, ameeleza kuwa msiba huo ni pigo kubwa maana waliishi kwa upendo kama familia na kuheshimiana na wadogo zake ambapo hata siku ya msiba walikubaliana yeye atangulie ili awapokee.

'Pigo la kupoteza watoto wanne kwa mpigo halielezeki'

“Tumepokea kwa masikitiko makubwa, wadogo zangu walikuwa wakinijali, walinipigia simu kila wakati kuulizia dada yao naendeleaje na hata tulipopata tatizo la mdogo wetu ambaye tulimzika jana  waliniambia dada tunakuja, wewe umetangulia maana mimi natokea Arusha, utupokee, nikawaambia tutakuwa pamoja, ni masikitiko, ni kitu ambacho hatuwezi kukizuia lakini tunamuomba Mungu atusaidie, atupe nguvu ili tumalize hili salama,” amesema.

Akizungumza Mchungaji Anituja Msuya amesema vifo hivyo ni pigo kubwa kwa familia na jamii kwa kuwa walikuwa ni watu wema na wenye upendo.

“Tumepokea msiba huu kwa masikitiko makubwa, ni jambo ngumu ambalo halipokeleki kirahisi, ila tunasema Mungu anabaki kuitwa Mungu, kwa sababu hatuna jambo lingine ambalo tunaweza kulifikiri, lakini tunafikiria kuwa Mungu ndiye aliyetenda haya na jina lake linabaki kubarikiwa na kutukuzwa,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msangeni Kassim Idd amesema tukio hilo limewashtua na kuwapa hofu kubwa na kwamba bado hawajaamini kama kweli limetokea licha ya kuona kwenye mitandao.

Naye Ahmed Msangi amesema tukio hilo limewapa taharuki kwa kuwa wakati linapotokea walikuwa katika msiba mwingine katika familia hiyo.

"Tukio hili limetupa taharuki, kwani tulichokuwa tunafahamu ni msiba wa kijana aliyefia Dar es Salaam kuja kuzikwa ambaye alizikwa jana, lakini cha kusikitisha jana tunakuja asubuhi tunapokea tena taarifa ya msiba wa vijana wanne wa Mzee Hashim uliotokana na ajali, tunaendelea kusubiri taratibu nyingine ili kuwapumzisha," amesema.