Video mamba aliyeuawa yaiibua Tawa

Muktasari:

  • Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori nchini (Tawa) imesema inafuatilia tukio la wawindaji maarufu kutoka Marekani, Josh na Sarah Bowmar kuua mamba mkubwa nchini.

Dar es Salaam. Taharuki imegubika tukio la wawindaji maarufu kutoka Marekani, Josh na Sarah Bowmar, baada ya kudaiwa kumuua mamba mkubwa zaidi duniani nchini Tanzania.

Wawili hao ambao pia ni wanandoa, wanadaiwa kumuua mamba huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 100, akiwa ndiye mwenye umri mkubwa zaidi duniani.

Mfululizo wa video za wanandoa hao na mamba huyo zimeshuhudiwa katika ukurasa wa mtandao wa Instagram wa Josh, alizochapisha zikionyesha mnyama huyo akining'inia juu ya mti.

"Nyie hamtaamini haya, mtazameni huyu mnyama mkubwa anayewindwa kwa uhuru wa asilimia 100 (free-ranging) hapa Tanzania," Josh ametamka kwenye kipande kimoja, akiwa na upinde na mshale mkononi.

Alifurahi zaidi, "Nimeua mamba kwa upinde na mshale, ni mkubwa zaidi ya wengine," amesema.

Katika kipande hicho cha video, Bowmar anadai iwapo vipimo vitafanyika, mamba huyo anaweza kuvunja rekodi ya kuwa mkubwa zaidi kuwahi kuwindwa.

Kinachotatanisha ni video inayoonyesha mamba aliyekufa akiburuzwa kwa kamba iliyofungwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser kabla ya kupandishwa kwenye mti.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Desemba 27, 2023, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori nchini (Tawa), Mabula Misungwi amesema wanafatilia tukio hilo.

"Nimeona hizo picha ila tutafatilia kujua ni sehemu gani uwindaji ulifanyika na tutatoa taarifa," amesema.

Historia yao

Wawili hao wamewahi kuhukumiwa kwa uwindaji haramu nchini Marekani

Gazeti la The Mirror la Uingereza, liliripoti wanandoa hao kutakiwa na Mahakama kulipa Sh350 milioni kama faini.

Mnamo mwaka wa 2016, Bowmars walipata umaarufu wa kimataifa kwa kumuua dubu mkubwa mweusi kwa mkuki wa walioutengeneza.

Wakosoaji wanasema kujivunia kuua na kupiga picha na wanyama walio katika hatari ya kutoweka kunaashiria kutozingatiwa kwa uhifadhi.

Mtaalam wa wanyamapori ambaye ameomba kuhifadhiwa jina amesema uwindaji wa mamba unaruhusiwa nchini Tanzania na muwindaji huyo ameitangaza nchi kuwa ina mamba wengi wakubwa.

Amesema katika mito mikubwa kama Mto Ruvuma, Mto Kilombero, Ruaha na Malagarasi kuna mamba wengi ambao ni hatari kwa binadamu hivyo ni muhimu kuwavuna ili wasaidie fedha za kigeni.

"Tanzania ni miongoni mwa nchi bora duniani ambazo zinatekeleza sheria za Shirika la kimataifa linalosimamia wanyamapori waliohatarini kutoweka (Cites) na tumekuwa tukipewa idadi ya kuwinda wanyama ambapo hata robo hatujawahi kuifikia," amesema.