VIDEO: Moto wateketeza ghala la kiwanda cha bora

Muktasari:
Moto ambao chanzo chake haujajulikana chanzo chake umetekeleza moja ya ghala la Kiwanda cha Bora jijini Dar es Salaam leo Alhamisi
Dar es Salaam. Moja ya ghala la Kiwanda cha Bora jijini Dar es Salaam limeteketea kwa moto leo Alhamisi Februari 28, 2019.
Moto huo ulioanza saa 11 alfajiri umeteketeza ghala hilo kwa kiasi kikubwa lililopangishwa kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi.
Mwananchi imefika kwenye kiwanda hicho na kukuta juhudi za kuzima moto huo zikiendelea sambamba na kujaribu kuokoa mali zilizopo kwenye maghala ya jirani.
Kamanda wa Jeshi la Zima Moto Wilaya ya Temeke, Michael Bachubila amesema hadi sasa wamefanikiwa kuzima moto huo kwa asilimia 50 na jitihada zaidi zinaendelea kumaliza ndani ya muda mfupi ujao.
“Kazi inaendelea na kama mnavyoona asilimia 50 tayari tumefanikiwa natumai ndani ya dakika 10 tutakuwa tumemaliza kabisa,” amesema
Bachubila ametoa rai kwa wamiliki wa viwanda na watu wanaokumbana na matukio kama ya moto kutoa taarifa mapema wanapoona cheche.
“Nitoe rai, ukiona cheche tu piga simu zimamoto tukiwahi kufika madhara yanapungua. Hawa wamechelewa walianza kupambana nao kupitia kampuni waliyoingia nayo mkataba,” amesema.
Zaidi ya magari saba ya zimamoto yalionekana katika eneo hilo yakipambana na moto huo ambao umesababisha moshi mzito barabara ya Pugu.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri