VIDEO: Siri mafanikio mwenye ulemavu wa macho aliyepata PhD

Muktasari:
- “Ulemavu ni gharama kubwa. Nimeajiriwa na ninalipwa sawa na waajiriwa wengine, lakini nalazimika kutoa sehemu ya kipato changu kuajiri mtu wa kunisaidia kusoma kazi za wanafunzi wangu wakati wa kupitia na kusahihisha kazi zao.”
Mwanza. “Ulemavu ni gharama kubwa. Nimeajiriwa na ninalipwa sawa na waajiriwa wengine, lakini nalazimika kutoa sehemu ya kipato changu kuajiri mtu wa kunisaidia kusoma kazi za wanafunzi wangu wakati wa kupitia na kusahihisha kazi zao.”
Hiyo ni kauli ya Dk Celestine Karuhawe, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Mwanza ambaye licha ya kuwa na ulemavu wa macho, amemudu kusoma hadi kuhitimu Shahada ya Uzamivu katika elimu.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jijini Mwanza jana, Dk Karuhawe alitaja rasilimali fedha, muda na watu kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazofifisha juhudi za watu wenye ulemavu kufikia malengo yao kimaisha.
“Maisha yangu ya masomo ya PhD ni mfano hai; kwa kweli yalikuwa ya kusumbua kidogo, haikutakiwa inichukue miaka saba kuhitimu, lakini hali yangu ya ulemavu na taratibu za chuo zilinifanya nihitimu baada ya miaka saba badala ya mitatu au minne kama wengine,” alisema Dk Karuhawe, akizungumzia milima na mabonde ya kuhitimu PhD kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Alisema licha ya utaratibu wa UDSM wa kuajiri watu wa kuwasomea vitabu wasioona na kuyaweka maandishi kwenye kompyuta yenye mfumo wa sauti, malumbano kati ya maprofesa wanapopitia kazi na machapisho huchelewesha wanafunzi kuhitimu.
“Kuna wakati mwanafunzi anatakiwa kuondoa baadhi ya mambo kutoka kwenye chapisho lake, lakini anapofanya hivyo na kuwasilisha upya kazi yake hutakiwa na mwingine kuyarejesha yale ambayo mwanzoni alitakiwa kuyaondoa; hii nayo inachelewesha watu kuhitimu,” alisema Dk Karuhawe, ambaye ni mume na baba wa watoto wanne.
Huku akimmwagia sifa mke wake, Beatrice na watoto wake, Devotha, Renata, Remidius na Castus kwa kumuunga mkono na kumtia moyo, Dk Karuhawe aliushukuru uongozi wa Saut kwa kumpa likizo ya malipo na kumtafutia mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
“Haikuwa jambo rahisi kusoma na kuhitimu katika umri wa utu uzima wa miaka 54 huku nikiwa mume, baba na mkuu wa familia ninayetegemewa,” alisema Dk Karuhawe akijibu swali la ugumu wa kusoma ukubwani.
Wanavyomtazama
Eveline Nyafurunjo, mmoja wa wanafunzi wa Dk Karuhawe katika kozi ya elimu Saut alisema mhadhiri huyo ni miongoni mwa nguzo zake muhimu katika masomo yake kutokana na aina ya ufundishaji wake unaohakikisha wanafunzi wanamwelewa.
“Dk Karuhawe ni kati ya wahadhiri wenye vipaji maalumu tulionao hapa chuoni. Licha ya uwezo wake wa kufundisha bila kuandika chochote ubaoni, pia amewakariri na kuwatambua wanafunzi wake kwa sauti na kuwagusa. Si tu nimefurahi kumwona akihitimu, bali pia sina shaka na PhD yake,” alisema Nyafurunjo ambaye sasa ni mhadhiri msaidizi kitivo cha Elimu Saut.
Naye Mkuu wa Idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma Saut, Dk Peter Mataba alisema kitendo cha Dk Karuhawe kutunukiwa PhD ni chachu ya maendeleo kielimu kwa wengi, huku akimshauri mwanazuoni huyo kuendelea hatua inayofuata ya uprofesa.
Soma gazeti la Mwananchi kesho kwa habari zaidi.