VIDEO: Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa, Ngoma bado mbichi

Dar/Moshi. Sintofahamu ya uchaguzi wa serikali za mitaa imeendelea baada ya vyama vya siasa vya upinzani kushikilia msimamo wa kujitoa licha ya Serikali kutoa tamko la kuwarejesha wagombea waliokuwa wameenguliwa.

Jana, Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo alitangaza kuwarudisha wagombea wa vyama vyote waliochukua na kurudisha fomu na baadaye kuenguliwa, lakini ni wale wanaokidhi vigezo.

Licha ya moja ya sifa ambazo mgombea anatakiwa kuwa nazo ni kudhaminiwa na chama chake cha siasa, Waziri Jafo alisisitiza kauli yake ya juzi kuwa Serikali inatambua wagombea wote walioomba bila ya kujali kama vyama vyao vimejitoa ili kutoa nafasi kwa wapiga kura kuchagua.

Vyama vya Chadema, ACT-Wazalendo, Chauma na NCCR-Mageuzi viliamua kujitoa kwenye uchaguzi huo kupinga vitendo vya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi, kama kuwanyima fomu, kutokuwepo ofisini kupokea fomu za wagombea wanaozirejesha na kuenguliwa kwa wagombea wao kinyume cha sheria. Pamoja na kauli ya Jafo ya kurudisha wagombea hao jana, vyama hivyo vimesisitiza kujitoa na pia kupinga uamuzi wa kuwarudisha wagombea wao.

Hata hivyo, vyama vya siasa na wanasheria wameitahadharisha Serikali kuwa uamuzi wa kulazimisha wagombea wa vyama vilivyojitoa ni kuingiza wagombea binafsi kwa mlango wa nyuma jambo ambalo ni hatari.

Mbali na wanasheria, Chadema ilienda mbali zaidi na kumtaka Jafo kuacha kuvunja Katiba na Sheria za nchi waziwazi.

Wakati hayo yakiendelea, NCCR-Mageuzi imetangaza kujitoa ikisema Serikali imeamua kuitoa kwa hila.

Akizungumzia na wanahabari jijini Dodoma jana, Waziri Jafo alisema jina la mgombea likishateuliwa linabaki kwenye karatasi ya kupigia kura hata kama vyama vyao vimejitoa kushiriki uchaguzi huo.

Kauli hiyo ya Jafo imepingwa na wanasheria na watetezi wa haki za binadamu, wakidai inavunja Katiba na sheria za nchi zinazotaka mgombea wa nafasi hizo za kisiasa kudhaminiwa na chama. Wanasheria hao wanadai ni kutokana na takwa hilo la kikatiba na kisheria, ndio maana kuanzia Rais, mbunge, diwani na viongozi wa serikali za mitaa ni lazima wadhaminiwe na chama cha siasa.

Chadema yashikilia msimamo

Wakati Waziri Jafo akitangaza kulegeza msimamo, Chadema imeshikilia msimamo wake wa kujitoa kwenye uchaguzi huo, ambao umekuwa ukikosolewa hata kabla ya mchakato kuanza.

Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam, naibu katibu mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika aliwataka wagombea waliopitishwa kuendelea kuwasilisha barua za kujitoa.

Mnyika alisema kanuni ya 14 na 15 za uchaguzi huo zinaelekeza kwamba mgombea lazima adhaminiwe na chama cha siasa, hivyo, kauli ya Waziri Jafo kuwatambua wagombea waliopitishwa ni upotoshaji.

“Sisi kama chama tutamwandikia barua Waziri Jafo kumpiga marufuku kulitumia jina la Chadema au nembo yake katika mchakato wa uchaguzi kwa sababu tumejitoa,” alisema Mnyika.

ACT Wazalendo

Msimamo wa kutorejea kwenye uchaguzi pia ulitolewa na kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alimtaka Waziri Jafo asimamishe mchakato huo kwa sasa.

“Hatutahalalisha haramu hata siku moja,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini.

“Mchakato wa uchaguzi uanze upya kwa kuundwa kamati huru ya kusimamia uchaguzi chini ya Tamisemi itakayokuwa na wajumbe kutoka vyama vyote vya siasa. Uchaguzi wa Novemba 24, ufutwe, itangazwe tarehe mpya na mchakato uanze upya,” alisema Zitto.

Kabwe alisema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Sheria ya Uchaguzi na kanuni zilizosainiwa na Jafo, mgombea anatakiwa kudhaminiwa na chama siasa.

NCCR-Mageuzi nao wajitoa

Katika hatua nyingine, chama cha NCCR-Mageuzi jana kilitangaza rasmi kujitoa katika uchaguzi huo kikidai ya kufanyiwa hujuma za wazi na wasimamizi.

Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alisema chama hicho kilikuwa na wagombea 35,407 waliochukua fomu nchi nzima, na waliofanikiwa kurejesha na zikapokelewa za wagombea 14,567 tu nchi nzima.

“Sasa katika mazingira ambayo ofisi za wasimamizi wasaidizi zilifungwa mathalani Jimbo la Vunjo ambako zilifungwa kwa siku nne, utasemaje mchakato huu ni huru na haki?” alihoji Mbatia.

Chauma

Naye mwenyekiti wa Chauma, Hashim Rungwe aliungana na msimamo wa wengine waliojitoa licha ya tamko la Waziri Jafo.

“Hayo ni maneno yake Jafo, lakini msimamo wa chama kutoshiriki uchaguzi huu upo palepale,” alisema Rungwe.

Lakini katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM anayehusika na uhusiano wa kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga alidai kuwa wapinzani wanawanyima wananchi haki kwa uamuzi wao wa kujitoa.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa CCM wa Wilaya ya Mkuranga jana, Lubinga alidai kuwa vyama hivyo havikuhoji wanachama wao.

“Wanachokifanya sasa (kususia uchaguzi) ni dalili za wapinzani kushindwa mwaka 2020,” alisema Kanali Lubinga.

“Mfano, ni wabunge na madiwani wao waliohamia CCM kwani waliondoka baada ya kuona mambo yasiyofaa yakiwemo haya yanayotokea.”

Wanasheria wanasemaje

Uamuzi wa kuwarejesha wagombea wakati vyama vyao vimejitoa pia ulipokelewa kwa mtazamo tofauti na wanasheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mkoani Kilimanjaro, David Shillatu alisema kuwarejesha wakati vyama vyao vimejitoa ni kukubaliana na wagombea binafsi.

“Bahati mbaya sana hatuna sheria ya mgombea binafsi nchini na angekuwepo labda hao wangeomba kusimama kama wagombea binafsi. Lakini muda huo ulishapita pia,” alissema.

Naye mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Nguruma aliitaka Serikali kuheshimu utawala bora na kuacha kulazimisha wagombea waliojitoa.

“Vyama hivi vimetoa taarifa mapema hata kabla ya majina rasmi ya wagombea kutoka, sasa unapolazimisha majina yao yawepo ni kuendelea kuvunja sheria na Katiba,” alisema Ole Nguruma.

Lakini wakili wa Haki Kwanza Adovates, Aloyce Komba alisema Jafo yupo sahihi kwa mujibu wa Sheria na kanuni za uchaguzi huo pamoja na kanuni zake zilizofanyiwa marekebisho mwaka huu.

“Vyama vya siasa vilivyojitoa kwenye mchakato huu, vilishatoa wagombea. Ndio maana nasema vilichelewa kujitoa kwa sababu wagombea wao walishaingia kwenye mchakato ikiwemo mchujo wa mwisho,” alisema Komba.

Hata hivyo, alisema Katiba iliyopo na sheria za uchaguzi zinafanya chama tawala cha CCM kuwa na nafasi kubwa ya kushinda katika chaguzi zote kwa sababu hakuna tume huru ya uchaguzi kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992.