VIDEO: Ukweli katazo la simu kesi ya kina Mbowe
Muktasari:
- Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Magdalena Ntandu, amefafanua sababu ya kuwepo kwa utaratibu mpya wa kusikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Dar es Salaam. Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Magdalena Ntandu, amefafanua sababu ya kuwepo kwa utaratibu mpya wa kusikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Akizungumza leo Alhamisi Septemba 16, 2021, Ntandu amesema wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na uwezo mdogo wa chumba cha mahakama ikilinganishwa na idadi ya watu wanaotaka kuingia.
Alisema kutokana na miundombinu ya mahakamani hapo, wamependekeza watu 48 tu waruhusiwe kuingia katika chumba cha mahakama kusikiliza kesi hiyo.
“Mahakama kama mahakama tunapenda watu wote waweze kuingia na kusikiliza kesi kwa sababu ni haki yao ya kujua kesi inaendaje mahakamani, hakuna katazo, kutokana na miundombinu ya hapa mahakamani hatuwezi kuhakikisha watu wote wameingia kwa sababu chumba hakitatosha,” amesema.
Mbowe na wenzake Halfani Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdilkahi Ling’wenya wanatuhumiwa kujihusisha makosa ya ugaidi na uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa nainu msajili huyo, mawakili 20 wa utetezi, mawakili wa Serikali nane, ndugu wa washitakiwa wasiozidi watano, watu wa ulinzi na usalama watano, wanahabari 10 na watu maalumu watatu ndio watakaoruhusiwa kuingia.