VIDEO:Wajawazito wakumbushwa chanjo ya polio

Wajawazito wakumbushwa chanjo ya polio

Muktasari:

Kesho Jumamosi Oktoba 24, 2020 ni siku ya polio duniani ambalo nchini Tanzania wajawazito wamekumbushwa kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanapewa chanjo ya ugonjwa huo kama inavyoelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Dar es Salaam. Kesho Jumamosi Oktoba 24, 2020 ni siku ya polio duniani ambalo nchini Tanzania wajawazito wamekumbushwa kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanapewa chanjo ya ugonjwa huo kama inavyoelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa kampeni ya kutokomeza polio klabu ya Rotary Mikocheni, Regina Mwengi walipotembelea Hospitali ya Mwananyamala kushuhudia  huduma ya utoaji chanjo hiyo  kwa watoto wachanga.

Amesema licha ya nchi kadhaa za Afrika kufanikiwa kukabiliana na ugonjwa huo, tahadhari zinatakiwa kuendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa wanakuwa salama.

Hata  Hivyo,  Klabu ya Rotery Mikocheni kesho itafanya maadhimisho hayo kwa kutembea kilomita zaidi ya 10 kuanzia saa 12 asubuhi eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili kuelimisha umuhimu wa athari zinazosababishwa na polio.

Ofisa muuguzi anayehusika na chanjo katika Hospitali ya Mwananyamala,  Pelagia Baturulimi amesema jitihada kubwa zinaendelea kufanyika kuhakikisha watoto wachanga wanakingwa dhidi ya ugonjwa huo.

Amesema kwa mwezi wanatoa chanjo kwa watoto 700 hadi 1200 wanaozaliwa ndani na nje ya hospitali hiyo.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Daniel Nkungu ameitaja klabu hiyo kama wadau wenye mchango katika jitihada za kutokomeza polio wakisaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa chanjo.

“Chanjo ni gharama kutengeneza, kuzisafirisha, kuzitunza na hata kuzisambaza, hivyo wadau kama hawa ni muhimu kwa kuwa wanawekeza nguvu zao katika kuhakikisha watoto wanapata chanjo na wanakuwa salama.”

“Hapa hatujawahi kuwa na kesi ya mtu mwenye polio kutokana na suala hilo kuchukuliwa kwa uzito mkubwa,” amesema Nkungu.