VIDEO: Wapinzani walitaka KKKT kutojibu barua ya Serikali

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (aliyekaa katikati) akiwa na wabunge wenzake wa kambi rasmi ya upinzani bungeni akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, kuhusu kambi hiyo kupinga barua serikali ya kulipa siku 10 Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)  kufuta waraka walizotoa kipindi cha Pasaka mwaka huu. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

KKKT ilitoa waraka wa Pasaka huku TEC wakitoa wa Kwaresima 

Dodoma. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imeliomba Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kutojibu barua waliyopewa na Serikali na kuitaka Serikali kuwaomba radhi waumini wa madhehebu hayo.

Wabunge hao wa upinzani wamesema kuanzia sasa watahakikisha wanatumia mbinu mbalimbali ndani ya Bunge kuitaka Serikali kutoa majibu ya kina kuhusu barua hizo hususan kuifuta barua yake.

Msimamo huo wa upinzani umetolewa leo Juni 7, 2018 na wabunge wa upinzani kwa pamoja katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

KKKT ilitoa waraka wa Pasaka huku TEC wakitoa wa Kwaresima na hivyo wametakiwa kufuta waraka huo ndani ya siku kumi kuanzia Mei 30, 2018.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia amesema Waziri Mkuu ndiyo msimamizi na mdhibiti wa shughuli za Serikali bungeni na swali lililoulizwa lilitaka kupata majibu kuhusu hatima ya KKKT na Katoliki.

Amesema, swali kwa Waziri Mkuu lilitaka kupata majibu  kwa kuwa makanisa hayo yameandikiwa barua ya kupewa siku kumi kufuta waraka wa Pasaka wa KKKT na  wa TEC uliotolewa kipindi cha  Kwaresima.

“Wasiwajibu Serikali halafu waone Serikali itachukua hatua gani kwani nchi hii si mali ya Serikali,” amesema Mbatia na kuongeza:

“Waumini wako katika hamaki, viongozi hawa wa dini ni Watanzania na wana haki ya kutoa maoni, Serikali inapaswa kuwaomba radhi waumini.”

Kaimu Kiongozi wa Upinzani Bunngeni, Abdallah Mtolea amesema viongozi wa siasa na wa kiroho wanaaminika kuliko wanasiasa.

“Tumeamua kuyasema haya, yanayofanyika kwa kuwa yanakwenda kuivuruga nchi hii, taasisi hizi zinaongozwa na viongozi wa kiroho wanaoaminika kuliko sisi wanasiasa,”amesema

Mtolea ambaye ni Mbunge wa Temeke (CUF) ameongeza:

 “Serikali iache kuingilia hizi taasisi, iache kuwaingilia pale wanaposema wanachanganya masuala ya siasa.”

Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amesema serikali inatakiwa kuufuta waraka huo.

“Tutahoji na tutatumia kanuni zote za Bunge kuitaka Serikali kutoa majibu yake na katika hili tutalifanya kwa umoja wetu.”

 “Kimsingi Serikali inapaswa kuifuta barua hiyo iliyoandikwa na Komba. Kwa kuonyesha hili ni kaa na moto kwa Serikali.”ameongeza