Vidonge vya P2, miso vyaendelea kuuzwa holela

Vidonge vya P2, miso vyaendelea kuuzwa holela

Muktasari:

  • Licha ya Serikali kutoa amri ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali wafanyabiashara wanaouza vidonge vya dharura vya kuzuia ujauzito ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu P2 na zile za kutoa mimba ‘Misoprostol’ bila cheti cha daktari, vimeendelea kuuzwa katika maduka ya dawa kiholela.

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kutoa amri ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali wafanyabiashara wanaouza vidonge vya dharura vya kuzuia ujauzito ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu P2 na zile za kutoa mimba ‘Misoprostol’ bila cheti cha daktari, vimeendelea kuuzwa katika maduka ya dawa kiholela.

Mwananchi limefanya uchunguzi katika maduka kadhaa ya dawa muhimu makubwa na madogo ndani ya jiji la Dar es Salaam na kubaini kila duka lilikuwa likiuza bidhaa hizo bila kuhitaji cheti cha daktari.

Gazeti hili lilishuhudia aina saba ya vidonge vya P2 vinavyozalishwa na viwanda mbalimbali vikiuzwa katika maduka ya dawa tofauti kwa bei ya Sh5,000 na vingine Sh10,000. Vidonge hivyo vipo vilivyogawanywa kwa vidonge viwili na aina nyingine ilikuwa na kidonge kimoja pekee.

Maduka yaliyotembelewa ni yaliyopo Mikocheni, Sinza, Survey, Tandale, Buguruni, Banana, Kinyerezi, Tabata na Mbezi.

Biashara ya vidonge vya Miso na P2 imekuwa ikifanyika kama magendo, kwani hazihifadhiwi kama dawa nyingine na wengi wa wauzaji walikuwa wakizitoa katika droo za makabati.

 Hata hivyo, baadhi ya wauzaji walisema wanauza bidhaa hizo kwa kificho kutokana na matamko mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na Serikali.

“Ninakuuzia hizi dawa usiruditena hapa, ninamalizia boksi lililokuwepo zinazuiwa sasa hivi sitazichukua tena,” alisema muuzaji mmoja Tabata.

Muuzaji katika duka la Buguruni alisema, “hizi dawa siyo nzuri, kwa nini unakunywa? Ungezaa tu huyohuyo unayefanya naye starehe ndiye atakayehudumia, madhara yake baadaye ni makubwa.”

 Hata hivyo, duka la dawa lililopo Tandale, muuzaji aliuliza iwapo mteja angependa kulipia bidhaa hiyo kwa fedha taslimu, kwa huduma za fedha kwenye simu au kwa scanner bila wasiwasi wowote.

Alipoulizwa kuhusu sakata hilo, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alisema kitengo chake kinahusika na utungaji wa sera, hivyo watekelezaji ambao ni Msajili wa Baraza la Famasia Tanzania ndiye anayetakiwa kulifanyia kazi hilo.

Msajili wa Baraza la Famasia nchini, Elizabeth Shekalaghe alisema tayari wameshaanza ukaguzi wa bidhaa hizo nchini. “Na sisi tuko kwenye ukaguzi.

Pamoja na kwamba mlikwenda kwenye famasi kubwa ambako tunaruhusu ziuzwe kwa cheti cha daktari, ugomvi wetu upo katika maduka madogo ambayo pia yanauza hizi dawa,” alisema Shekalaghe.

Akitoa hotuba wakati wa mkutano mkuu wa chama cha wafamasia (PST) wiki iliyopita, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima aliagiza hatua kali zichukuliwe kwa wote wanaokiuka taratibu ya kanuni ya vyeti vya dawa na kuacha kuweka maisha ya Watanzania kwenye hatari.

“Iweje dawa zinazohitaji cheti cha daktari zitolewe kinyume na kanuni, chukueni hatua kali kwa wote wanaokiuka, aidha rekebisheni sheria na kanuni zinazodhibiti suala la uandikaji na utoaji wa vyeti vya dawa,” alisema Dk Gwajima.