Vifo vya Maria na Consolata vyagusa kila kona

Sunday June 03 2018
Pacha pic

Dodoma. Kifo kinaleta huzuni lakini hakizuiliki. Ndivyo unavyoweza kusema ukimshukuru Mungu kwa yote katika kipindi hiki cha huzuni kufuatia vifo vya pacha wa kipekee wa Tanzania walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti.

 

Pacha hao walifariki dunia jana Juni 2, 2018 katika hospitali ya mkoa wa Iringa, huku taarifa zilizothibitishwa na mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela, zikibainisha kuwa pacha hao wamefariki wakipishana kwa takribani saa 2.

 

Kifo hakizoeleki na kila kinapotokea watu huwa na huzuni, kukumbuka mengi yaliyofanywa na aliyetangulia mbele za haki. Rais John Magufuli ni miongoni mwa wengi walioshtushwa na vifo vya pacha hao na kutoa salamu za rambirambi kupitia  mtandao wa kijamii wa Twitter, jambo ambalo limefanywa na watu wengine wengi kupitia mtandao huo na mingine ya  Instagram na facebook.

 

Advertisement

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, kiongozi mkuu huyo wa nchi ameandika, “Nimesikitishwa na kifo cha Maria na Consolata. Nilipokwenda hospitali waliliombea Taifa. Walikuwa na ndoto ya kulitumikia Taifa.”

 

“Poleni familia, Masista wa Maria Consolata na wote walioguswa. Pumzikeni  mahali pema wanangu. Bwana alitoa na bwana ametwaa jina la bwana lihimidiwe.”

 

Katika mtandao huo wa Twitter, Naibu Spika Dk Tulia Ackson ameambatanisha picha aliyopiga na pacha hao alipokwenda kuwatembelea hospitali walikokuwa wamelazwa.

 

“Poleni sana wazazi na walezi wa watoto hawa. Hakika ni watoto ambao waliweza kutufundisha kutokata tamaa kwenye maisha na kumshukuru Mungu kwa kila jambo, tutawakumbuka daima Maria na Consolata kwa alama mliyoiacha, Mungu awapumzishe kwa amani,” amesema.

 

Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete huku akiambatanisha picha ya pacha hao amesema, “Hebu angalia tabasamu lao...ghafla ulimwengu umefunga macho na wameachwa katika dunia nyengine. Mungu fundi, Mungu mjuzi, Mungu mpangaji, pumzikeni kwa amani watoto wazuri...R.I.P Mapacha wasomi.”

 

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameandika , “hakika vita wamepigana, mwendo wameumaliza. Wapumzike kwa amani Maria na Consolata. Natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki.”

 

Katika ukurasa wake wa Twitter, Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema, “Nautafakari wasaa wa mwisho wa watoto Maria na Consolata, nauona uchungu wa yule aliyebaki hai, akitanguliwa na mwenzake.”

 

“Wamepigania uhai wao hadi dakika ya mwisho. Mungu awape pumziko la amani. Ni msiba mkubwa kwa Taifa letu. Poleni wote mlioguswa na msiba huu.”

 

Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu Profesa Jay ameandika katika Instagram yake na kuambatanisha picha akisema, “Dah wapendwa wetu mapacha Maria na Consolata wametangulia mbele za haki. Raha ya milele uwape eeh bwana na mwanga wa milele uwaangazie, wapumzike kwa amani, amani.”

 

Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amesema, “nimepokea kwa masikitiko makubwa sana msiba wa mabinti zetu na wadogo zetu (mapacha walioungana Consolata na Maria) ambao wamefariki Dunia katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa walipokuwa wakitibiwa.”

Msanii wa Bongo Movie, Steven Mengere maarufu kama Steve Nyerere katika Instagram ameandika, “hatuna budi kusema kazi ya Mola haina makosa. Nichukue nafasi hii kuwapa pole ndugu jamaa na familia pamoja na Watanzania wote walioguswa na msiba huu, hakika sisi tuliwapenda kwa namna moja ila Mungu amewapenda zaidi.”

Soma: Pacha maarufu walioungana, Maria na Consolata, wafariki dunia

 

Advertisement