Prime
Vijana wanavyopasua vichwa viongozi Tanzania

Muktasari:
Tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini limezidi kuwapasua vichwa viongozi wa kitaifa ambapo kwa nyakati tofauti wametoa maelekezo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri kupitia fursa zilizopo mbele yao.
Dar/mikoani. Tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini limezidi kuwapasua vichwa viongozi wa kitaifa ambapo kwa nyakati tofauti wametoa maelekezo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri kupitia fursa zilizopo mbele yao.
Tanzania, yenye idadi ya watu milioni 61, inajumuisha makundi rika tofauti, huku nguvu kazi ikiwa ni vijana, wakiwemo waliopata elimu katika ngazi tofauti na ambao hawakuipata, hali inayoibua maswali na mijadala lukuki.
Mijadala hiyo inashika kasi hasa kutokana na kauli za viongozi waandamizi wa Serikaki -- Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ndani ya siku tatu wametoa kauli mbalimbali kuwahusu vijana hao.
Juzi, akifunga Maonyesho ya Nanenane yaliyofanyika mkoani Mbeya, Rais Samia alizungumzia namna vijana waliomaliza masomo wanavyokosa kazi licha ya kupatiwa ujuzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Vijana wetu hawa wamemaliza shule wakawa wanazubaa tu huko, wengi wao wamekwenda JKT lakini wakitoka hamna kazi, wapo tu lakini ni nguvu kazi nzuri, wamefunzwa maadili JKT, ni vijana wazuri kwa Taifa, wamefunzwa uzalendo, hawana cha kufanya.
“Kazi ni kuhamia Twitter Republic watutukane kule na tunastahiki kwa sababu tumewasomesha, hawana kazi za kufanya,” alisema Rais Samia alipotembelea banda la ufugaji wa ng’ombe kwenye maonyesho hayo.
Aliipongeza Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwachukua vijana wanaotoka JKT na kuwafundisha stadi za kilimo na ufugaji kupitia mradi wa BBT unaolenga kuongeza ajira kwa vijana katika sekta za kilimo na ufugaji.
Kwa upande wake Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati akifungua kongamano la vijana mkoa wa Dodoma Jumatatu, mbali na kuagiza mambo matano kwa halmashari za wilaya nchini, ikiwemo kuwaunganisha vijana katika uzalishaji mali na kuwa na kanzidata za kuwatambua, aligusia changamoto zao.
“Ni neno lenye ukakasi kulisema lakini ngoja niseme tu, kwamba vijana wengi wa nchi yetu maadili yao yameporomoka, wengi hawana uzalendo na Taifa lao, hawana uadilifu, ni wavivu na wamejawa na tamaa ya kupata fedha kwa haraka,” alisema Dk Mpango.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akifunga kongamano hilohilo juzi, aliwataka viongozi na wataalamu katika mamlaka za Serikali za mitaa kuweka kipaumbele katika kuendeleza vijana ili washiriki kikamilifu kwenye shughuli za kuinua uchumi na kuwapatia ujuzi na mbinu za ujasiriamali.
Pia, Majaliwa alisisitiza kila mkoa kuandaa mpango mahsusi wa kuhamasisha vijana kufanya shughuli zenye staha na kuwavutia wengi kushiriki shughuli za kiuchumi katika maeneo yao kama ilivyofanya Dodoma
“Kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki katika kuwapa taarifa kuwaongoza na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kukuza mitaji yao.
“Halmashauri zihakikishe kuwa vijana walio tayari kufanya uwekezaji katika shughuli za uchumi wanapata taarifa za fursa za mitaji. Nyote mlimsikia Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akisisitiza kuhusu kutoa taarifa kwa walengwa,” alisema Majaliwa.
Mitazamo ya wadau
Wakati viongozi wakisema hayo, Profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abel Kinyondo alisema matamanio yake ni kuona vijana wanawezeshwa zaidi kwenye taaluma na fani za kisasa ambazo ndizo zilizopo kwenye soko la dunia.
Alisema kulingana na mwelekeo wa dunia sasa, kazi nyingi zilizopo sokoni zinahusu matumizi ya Tehama, hivyo ni vizuri vijana wakawezeshwa kwenye fani kama akili bandia, dijitali na si kwenye kilimo ambako tayari kuna watu wanaohitaji kusaidiwa.
“Kazi nzuri ni zile zisizo na mipaka ambazo ni za kidijitali, mfano mtu unaweza ukawa Dar es Salaam ukaajiriwa na kampuni iko Marekani. Hivyo tuchague aina ya ajira ambazo soko linawahitaji, tuangalie zaidi duniani na si hapa Tanzania,” alisema Profesa Kinyondo.
Kwa upande wake Israel Ilunde, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Ushirikiano wa Vijana (YPC), alisema kauli za viongozi zinaonyesha dhamira njema ya kuwasaidia japokuwa si ngeni.
Alisema Serikali inapaswa ishirikiane na wadau mbalimbali katika kutekeleza hilo la kuwawezesha vijana.
“Ni mtazamo mzuri wa kuwasaidia vijana kwa sababu ndiyo tegemeo la nchi, hivyo wanapaswa wapewe mikopo kwa wakati pamoja na elimu ya matumizi yake na bajeti ya vijana itekelezwe ili wigo wa kuwasaidia uwe mpana,” alisema Ilunde.
Alisema katika kufanikisha hilo, Serikali inapaswa ishirikiane na vijana wenyewe, taasisi binafsi, asasi za kiraia pamoja na taasisi za kifedha.
Jambo hilo pia lilimwibua Abdul Nondo, mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, aliyesema kwanza Serikali inapaswa iwatambue hao vijana wako wapi na wanajishughulisha na nini.
Alisema katika kila mkoa kuna shughuli za uzalishaji mali, akitolea mfano Mkoa wa Kigoma ambao kuna vijana wanalima na wengine wanajishughulisha na uvuvi, ambao wanahitaji msaada ili waweze kuendelea.
“Kuna kundi la vijana ambalo linajishughulisha na shughuli za kiuchumi linahitaji msaada wa kimtaji ili liweze kuendelea kulingana na aina ya uzalishaji wa eneo husika,” alisema Nondo.
Alisema jambo kubwa ni kuwapatia mtaji, huku akionyesha wasiwasi juu ya kauli za viongozi kuhusu kuwainua vijana, akizitaja kuwa za “kawaida majukwaani”.
Walichokisema vijana wenyewe
Theophil Emmanuel, mkazi wa Bulangwa wilaya ya Bukombe alisema tatizo la ajira kwa vijana linaongezeka kutokana na wingi wa wahitimu wa vyuo vikuu kukosa stadi za kazi, huku baadhi yao wakibagua ajira au kazi zinazopatikana, ikiwemo za ujasiriamali, kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Serikali irekebishe mitalaa kwa kuingiza elimu ya ujasiriamali na kujitegemea kuanzia ngazi ya msingi ili kuwezesha wahitimu kujiajiri na kutengeneza fursa za ajira badala ya kutegemea kuajiriwa,” alisema.
Mkazi wa Kata ya Mwasekwa jijini Mbeya, Andrew Sayota alisema kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwenye taasisi za Serikali kunachangia vijana kukosa fursa za ajira na kujikuta wakijiingiza kwenye vitendo vya uvunjifu wa maadili katika jamii.
Adela Madyane, mkazi wa Kigoma alisema suala la mmomonyoko wa maadili linatokana na vijana kukosa ajira, hali inayowasababisha kujiingiza katika mambo yasiyo na maadili kama dawa za kulevya ili kujipatia kipato.
Kwa upande wake, Paul Makanyaga, mkazi wa manispaa ya Shinyanga, alisema hali hiyo imesababishwa na Serikari kufumbia macho masuala ya kubeti, kwani vijana wengi hawafanyi kazi, badala yake wanaenda kubeti na kusikiliza matangazo ya waganga.
Sisty Mushi, mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro alisema vijana hawajakata tamaa ila changamoto za maisha ndizo zinazosababisha.
“Sisi vijana kuwa na tamaa, maana umempa kijana elimu, amesoma hadi kuhitimu chuo kikuu, lakini yuko mtaani hana ajira, hivyo anatafuta njia ya kumwezesha kupata kipato cha kujikimu na ndiyo maana pia wengi wamejiingiza kwenye kamari,” alisema.
Naye Eppifania Emmanuel, mkazi wa Mkolani jijini Mwanza alisema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linasababishwa na wahitimu wengi kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu kukosa elimu ya ujasiriamali na ubunifu wa kujiajiri na kutengeneza fursa za ajira kwa wengine.
“Mmomonyoko wa maadili ni matokeo ya malezi na makuzi mabaya. Wazazi wengi hawana muda wa kukaa na watoto wao kutokana na kubanwa na shughuli za utafutaji mali, hali inayosababisha watoto kulelewa na wasaidizi wa kazi za nyumbani,” alisema.