Vikwazo vinne vyakwamisha mpango wa kupinga ukatili

Saturday May 21 2022
vikwazo pic

Kiongozi wa Mila Mbeya Mjini na Vijijini, Rocket Mwashinga 'Chifu Mwashinga' akieleza jambo wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mpango mkakati wa mawasiliano wa kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na watoto mkoani Mbeya.

By Saddam Sadick

Mbeya. Mtazamo hasi, ushirikiano mdogo kwa jamii, imani za kishirikina na bajeti ndogo vimetajwa kuwa kikwazo mkoani Mbeya katika kudhibiti ukatili wa Wanawake na watoto kwa kipindi cha mwaka uliopita, huku serikali mkoani humo ikiandaa mkakati mpya kukabiliana na matukio hayo.

 Akizungumza leo Jumamosi Mei 21, 2022 katika kikao cha kujadili utekelezaji wa mpango mkakati wa mawasiliano wa kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dk Vicent Anney amesema wameshindwa kufikia malengo waliyokuwa wameweka.

Amesema Mkoa huo ulikuwa umeweka mkakati kukomesha ukatili huo lakini hadi sasa wamefikia asilimia 40 tu, huku vikwazo ikiwa ni mfumo wa mtizamo hasi, ushirikiano mdogo kwa jamii na bajeti na imani za kishirikina hususani kwa wananchi.

"Tumeanza kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na makongamano na kuongeza bajeti katika mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu ili kuhakikisha tunatimiza malengo kwa sababu vitendo hivi vimekithiri sana, lazima tupate muarobaini" amesema Dk Anney.

Dk Anney ameongeza kuwa kwa kipindi cha miezi tisa jumla ya matukio ya ukatili 753 yameripotiwa huku ukatili wa shambulio la mwili likiongoza ikifuatiwa ubakaji na mimba na kwamba Mkoa huo umejipanga kuchukua hatua kali kwa atakayebainika na matukio hayo.

"Hadi sasa tunamshikilia Mwalimu mmoja aliyempa mwanafunzi na rafikia yake mimba, wengine wanne wakiwa kwenye uchunguzi na mmoja akiendelea kusakwa baada ya kukimbia, matukio haya yanashtua kwa sababu ndani ya miezi tisa kesi zilizopelekwa mahakamani ni 210 na mimba 163" amesema Dk huyo.

Advertisement

Kwa upande wake kiongozi wa mila, Rocket Mwashinga amesema mara kadhaa wamekuwa wakikosa ushirikiano kwa viongozi wa vijiji wakidhaniwa kuwa ni wachawi na kusema kuwa hali hiyo imewapa changamoto kubwa kufikia malengo.

"Ushirikiano muda mwingine kwa sisi machifu imekuwa changamoto, baadhi ya viongozi wa vijiji wamekuwa wakitunyima ushirikiano wakihisi sisi ni wachawi, niwaambie kwamba uchifu kama una dalili za wizi, uzinzi au uchawi huwezi kuupata, hii fimbo itakukataa" amesema Mwashinga ambaye ni chifu wa Mbeya Mjini na Vijijini.


Naye mwenyekiti wa kamati ya utendaji kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Mbeya, Padri David Sichinga amesema wao kama viongozi wa dini wanalaani sana matukio ya aina yoyote ya ukatili huku akieleza kuwa wamekuwa wakihubiri sana na kutoa mafundisho kwa waumini katika kuepuka vitendo vya kikatili.

"Hatupendi kuona matukio haya yanatokea sisi viongozi wa dini tumekuwa tukihubiri sana na kutoa mafundisho kwa vikundi vya kina Mama na vijana juu ya malezi bora lengo ikiwa ni kuondokana na vitendo hivi"amesema Sichinga.

Advertisement