Vilio, simanzi vyatawala ibada ya mazishi ya watu saba waliofariki kwa ajali Hai

Muktasari:

  • Watu hao saba walifariki papo hapo katika ajali ya magari iliyotokea eneo la Saweni wilayani Same katika barabara kuu ya Tanga – Moshi, majira ya saa 10:30 jioni Oktoba 11, 2022 wakitokea mkoani Tanga kulekea Moshi.

Hai. Miili ya watu saba ya familia moja ukiwamo wa ofisa uhamiaji katika uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) imewasili nyumbani kwa marehemu Sylvester Chambo, eneo la Kengereka wilayani Hai mkoani Kilimanjaro na kuibua vilio na simanzi.

Miili hiyo iliwasili nyumbani hapo majira ya saa 8:00 mchana kwa kubebwa na gari la polisi lenye namba PT 4277 aina ya Canter na kusababisha vilio vya maelfu ya waombolezaji waliofika nyumbani hapo.

Katika ibada ya mazishi ya marehemu hao iliyoongozwa na Padri Faustine Furaha wa parokia ya Hai katika jimbo Katoliki la Moshi, simanzi iliongezeka zaidi kila Padri alipokuwa akitaja majina ya waliofariki.

Watu hao saba walifariki papo hapo katika ajali ya magari iliyotokea eneo la Saweni wilayani Same katika barabara kuu ya Tanga – Moshi, majira ya saa 10:30 jioni Oktoba 11, 2022 wakitokea mkoani Tanga kulekea Moshi.

Ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T618 AWP aina ya ya Toyota Corolla likiendendeshwa na Sylvester Chambo aliyekuwa akitokea Tanga kuelekea Moshi na gari namba T515 DMV aina ya Voxywagen likitokea Moshi kuelekea Dar es salaam.


Jana, Oktoba 12, 2022, kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa,aliwataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Slyvester Chambo (36), Noel Semlingwa(33), mfanyabiashara wilayani Hai na John Mazengo, mwanafunzi wa kidato cha tatu na mkazi wa Moshi.

Wengine ni mwanafunzi darasa la nne, Calvin Slyvester, mwanafunzi wa darasa la tatu, Ester Moris, mwanafunzi wa darasa la sita, Calvin Slyvester na Alice Semlingwa, wote wakiwa wakazi wa Moshi.

Katika ibada hiyo ilihudhuriwa na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, mwenyekiti wa CCM mkoa, Patrick Boisafi, mkuu wa wilaya ya Hai, Juma Irando na mwenyekiti wa halmashauri ya Hai, Edmund Rutaraka.

Wengine ni pamoja na kamanda wa polisi mkoani hapa, Simon Maigwa, mkuu wa uhamiaji mkoa wa Kilimanjaro, Edward Mwenda pamoja na maofisa wengine wa jeshi la uhamiaji na wa serikali.