Viongozi Simiyu wafanya ibada kumuombea Magufuli

Viongozi Simiyu wafanya ibada kumuombea Magufuli

Muktasari:

  • Viongozi wa dini Mkoa wa Simiyu wamefanya ibada ya kumuombea Hayati John Magufuli.


Simiyu. Viongozi wa dini Mkoa wa Simiyu wamefanya ibada ya kumuombea Hayati John Magufuli.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa na wananchi, watendaji wa Serikali na wanachama wa CCM  wakiongozwa na mjumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho,  Emmanuel Gungu ilifanyika kwenye viwanja vya CCM wilayani Bariadi mkoani humo.

Akizungumza katika ibada hiyo, Gungu amesema Magufuli amefanya kazi kubwa hasa kuwaletea wananchi maendeleo.

"Hapa Simiyu Magufuli amefanya mambo mengi. Ametujengea barabara za lami, miradi mikubwa ya maji pamoja na viwanda," amesema  Gungu.

Naye Katibu wa CCM Mkoa Wa Simiyu, Hawra Kachwamba amesema Watanzania wanapaswa kumuenzi Magufuli kwa mambo mengi mema aliyofanya kwa Watanzania.

Shekhe wa Mkoa wa Simiyu Mahamud Kalokola amesema kiongozi huyo alifanya mengi hasa kwa  wanyonge ambao kwa kiasi kikubwa alikuwa akiwatetea.

"Magufuli amefanya mambo makubwa, alikuwa mtetezi wa wanyonge. Kikubwa tumuombe huko aliko mungu ampunguzie adhabu ya kaburi," amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga amesema Magufuli alijipambanua kuwa mtetezi wa wanyonge ni vyema Watanzania wakaendelea kumuenzi na kumkumbuka kwa mema aliyoyafanya.