Viongozi wa dini watakiwa kuliombea Taifa

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah (kushoto) na Rais wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation Sheikh Shariff Abdulqadir wakiomba dua wakati walipohudhuria hafla ya uzinduzi wa mashindano makubwa zaidi ya 22 ya Qur'aan Tukufu Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Aprili 17 mwaka huu.
Muktasari:
Viongozi wa dini wametakiwa kuendelea kuiombea nchi kuwa na utulivu na amani kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Dar es Salaam. Viongozi wa dini wametakiwa kuendelea kuiombea nchi kuwa na utulivu na amani kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa jana na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemedi Abdalla alipokuwa katika uzinduzi wa mashindano ya 22 ya uhifadhi wa Qur'an yaliyoandaliwa na taasisi ya Al-Hikma Foundation jijini Dar es Salaam yanayotarajiwa kufanyika 17 April 2022 katika viwanja vya Uhuru na Mkapa.
"Viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika katika kuhimiza amani, kukiwa na amani na utulivu hata shughuli za kimaendeleo zitakwenda vizuri,"alisema.
Aidha alitumia fursa hiyo pia kuwapongeza waandaaji wa mashindano hayo na kutoa wito kwa taasisi nyingine za kidini kuiga mfano huo.
Alisema mwitikio mkubwa wa watu kushiriki na kuhudhuria katika mashindano hayo kunaonyesha wazi wamehamasika kukisoma na kuhifadhi kitabu hicho kitakatifu cha Qur’an.
Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki alisema kuwa katika mashindano hayo ya mwaka huu ambayo ni ya 22 yanatarajia kupata washiriki kutoka nchi 22 huku nchi ya Tanzania ikiwakilishwa na washiriki wawili, mmoja kutoka Tanzania Bara na mwengine kutoka Zanzibar.
"Mshindi wa kwanza katika mashindano haya itakuwa Sh20 milioni,"alisema.
Alisema lengo la kuanzisha mashindano hayo mbali na kupata baraka za Mungu vilevile ni kuongeza Idadi ya watu waliohifadhi kitabu hicho kitakatifu.
"Mashindano hayo yamesaidia sana kuongeza idadi ya waliohifadhi Quran, awali katika kipindi cha ramadhani tulikuwa tunaleta maimamu kutoka Mombasa lakini hivi sasa wao ndio huchukua maimamu kutoka kwetu,"alisema.
Aliongezea kuwa pia yamelenga kuirudisha jamii katika maadili ya kumcha Mungu.