Viongozi wa dini watoa msimamo chanjo ya corona

Viongozi wa dini watoa msimamo chanjo ya corona

Muktasari:

  • Viongozi wa umoja wa dini mbalimbali umesema msimamo wao katika mapambano ya ugonjwa wa Covid-19 ni kusikiliza sauti za wataalamu na wanasayansi ikiwemo maamuzi ya chanjo ya kupambana na ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Viongozi wa umoja wa dini mbalimbali umesema msimamo wao katika mapambano ya ugonjwa wa Covid-19 ni kusikiliza sauti za wataalamu na wanasayansi ikiwemo maamuzi ya chanjo ya kupambana na ugonjwa huo.


Kauli ya viongozi hao imekuja siku chache baada ya chanjo zaidi ya milioni 1 za Covid - 19 kuwasili nchini, huku Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuzindua chanjo hiyo kesho kwa kuchanjwa Ikulu jijini Dar es Salaam.


Hayo yamesemwa leo Jumanne Julai 27, 2021 Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Amani, Mwashamu Askofu Nelson Kisare wakati akizindua mjadala wa nafasi ya taasisi za dini na wadau juu ya elimu ya umma katika tokomeza Covid-19.


“Msimamo viongozi wa dini ni kuikubali chanjo na kwanini tunakubali chanjo? Kwa sababu Rais aliunda timu maalum ya wanasayansi kumshauri na kufanya uchunguzi njia ipi itatufaa.


“Mungu amesema watu wangu wanapotea kwa kukosa maarifa na katika hili maarifa ni chanjo. Katika hili chanjo ipi? Tumekubaliana tusikilize sauti za wataalamu kuna vyombo vimetumwa kufanya tafiti na kutoa taarifa sahihi watakaosikia kwa hiyari yao wanaweza kuchanjwa,” amesema Askofu Kisare.


Amesisitiza kuwa viongozi wa dini zote wameafiki kuwa wanataka kusikiliza sauti ya wataalamu, “wanasemaje tutasikia watakaposhauri baada ya kufanya tafiti mbalimbali na tutawashauri watu watumie chanjo ambazo ni sahihi.”
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Hamis Makata amesema,


“Viongozi wa dini tumekubaliana kufuata miongozo ya Wizara ya Afya, kuitekeleza kwa vitendo iliwemo kuhimiza waumini kunawakwa maji tiririka na sabuni, vipima joto na kikubwa tunataka kulinda uhai wa watu wetu na chanjo ni muhimu.”