Viongozi wa kijiji matatani wakidai rushwa Sh150,000

Muktasari:
- Washtakiwa hao wanadaiwa kuomba rushwa hiyo 000 kutoka kwa Ally Mpemba, ili wamuachie huru kuishi kijijini hapo baada ya kukaidi amri ya baraza la wazee.
Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imewafikisha mahakamani watu watatu akiwemo ofisa mtendaji wa kijiji cha Nampalahala kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.
Washtakiwa waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Bukombe ni pamoja na ofisa mtendaji wa kijiji cha Nampalahala, Peter Ologwanannke, Mabula Ngoloban ambaye ni mhasibu wa baraza la wazee wa kijiji cha Nampalahala pamoja na Ruben Msabila, mjumbe wa baraza hilo.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Bahati Chitepo, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Chali Kadeghe alidai kuwa Novemba, 2023 washtakiwa hao walitenda kosa la kuomba na kupokea rushwa, kinyume na kifungu cha 15(1)(a)(b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Katika kesi hiyo namba 6684 ya mwaka 2024 washtakiwa hao wanadaiwa kuomba rushwa ya Sh150,000 kutoka kwa Ally Mpemba na kwamba walipokea Sh100,000 kama hongo, ili wamuachie huru kuishi kijijini hapo baada ya kukaidi amri ya baraza la wazee.
Washtakiwa wamekana kutenda tuhuma hizo n wako nje kwa dhamana, baada ya kutimiza masharti ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini fungu la dhamana ya Sh1 milioni. Kesi imeahirishwa hadi Machi 20, 2024 washtakiwa watakaposomewa hoja za awali.