Viongozi wamlilia Rais Magufuli

Viongozi wamlilia Rais Magufuli

Muktasari:

  • Viongozi mbalimbali wa kisiasa wametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa kisiasa wametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo cha Rais Magufuli saa tano usiku akisema kimetokana na tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.

“Machi 14 mwaka huu, alijisikia vibaya akakimbizwa Hospitali ya Mzena ambako aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hadi umauti ulipomkuta,” amesema Mama Samia.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameandika, “kwa masikitiko makubwa Machi 17, 2021 saa 12 jioni tumempoteza Rais John Magufuli ambaye amefariki kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.”

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe naye ametoa salamu zake za rambirambi akieleza kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Rais Magufuli huku akitoa pole kwa mama Janeth Magufuli pamoja na familia yake.

“Natoa pole kwa Samia Suluhu Hassan kwa msiba huu mzito kwa Taifa letu. Katika nyakati hizi za majonzi makubwa, tunamtakia kheri, ujasiri na ushupavu katika kutekeleza majukumu yake,” amesema Zitto katika taarifa yake.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa naye ameandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina.”

Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Akwinum Adesina ameandika katika mtandao wa Twitter: “Nimesikitishwa na kifo cha rafiki yangu na kaka yangu, Rais John Magufuli. Kiongozi thabiti. Alifanya kazi bila kuchoka kwa maendeleo ya Tanzania. Nitakukumbuka sana kwa jitihada zako za kuleta maendeleo Afrika.”

Mwanamitindo maarufu, Flaviana Matata naye ameandika: “Tumwinue Mama Samia katika maombi.” Pia, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba, Barbara Gonzalez ameandika: “Mpendwa wetu, Rais John Magufuli amekufa mapema kabla ya wakati wake. Mungu alilaze roho yake mahali pema peponi.”

Mbali na salamu hizo za watu mbalimbali, vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vimeripoti taarifa ya kifo cha kiongozi huyo na kueleza misimamo yake enzi za uhai wake.

Rais Magufuli amefariki akiwa na umri wa miaka 61 akiwa ametawala kwa miaka karibu sita tangu alipochaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 2015. Pia, alishinda uchaguzi wa Oktoba 28 mwaka jana kwa muhula wake wa pili ambao hajaumaliza.

Viongozi wamlilia Rais Magufuli

Mama Samia ametangaza siku 14 za maombolezo ya kifo chake ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti wakati taratibu za mazishi zikiandaliwa.